NEWS

Tuesday 4 October 2022

Rais Samia kuhutubia Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani



Na Mwandishi Wetu, Arusha
---------------------------------------

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa Mkutano wa 65 wa Shirika la Utalii Duniani Kamisheni ya Afrika (65th UNWTO-CAF Meeting), utakaoanza kesho Oktoba 5, 2022 katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Dkt. Pindi Chana (katikati pichni juu), katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika leo jijini Arusha.

Waziri Chana amesema mkutano huo utajadili kuhusu mustakabali wa ustawi wa maendeleo ya sekta ya utalii barani Afrika, hasa baada ya athari za mlipuko wa janga la UVIKO-19, iliyokuwa imeathiri utalii wa kimataifa kwa wastani wa kati ya asilimia 50 na 85 katika nchi mbalimbali, ikiwemo Tanzania.

Aidha, amesema mkutano huo ni muhimu kwa kuwa ni mojawapo ya jitihada za Serikali katika kuongeza idadi ya watalii na kutanua wigo wa mazao ya utalii nchini kupitia uendelezaji wa mazao ya utalii ya kimkakati, hususan Utalii wa Mikutano na Matukio.

Vilevile, ameweka bayana kuwa mkutano huo utawezesha kujengea uwezo wataalamu na wadau wa utalii katika kutangaza utalii, kuendeleza na kufungamanisha mazao ya utalii katika kanda mbalimbali za utalii nchini, kulingana na shabaha ya kuongeza idadi ya watalii hadi kufikia milioni tno na mapato ya Dola za Marekani bilioni sita ifikapo mwaka 2025.

“Mkutano huo ni nyenzo mojawapo ya kuunga mkono jitihada za Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi, kupitia programu ya Tanzania - The Royal Tour,” Balozi Chana amesema.

Mkutano huo wenye kaulimbiu ya “Kuujenga Upya Utalii Stahimilivu wa Afrika kwa Maendeleo Jumuishi ya Kiuchumi na Kijamii”, utahudhuriwa na Katibu Mkuu wa shirika hilo, Zurab Pololikashvili.

Pia utakutanisha mawaziri wenye dhamana ya masuala ya utalii na maliasili kutoka nchi wanachama wa UNWTO wa Kanda ya Afrika zaidi ya 50 na wadau wengine, wakiwemo wataalamu wa utalii na ukarimu katika ngazi ya kimataifa na kikanda, watoa huduma mbalimbali katika mnyororo wa utalii, wawekezaji na watu mashuhuri zaidi ya 150.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages