NEWS

Monday 24 October 2022

Uzalishaji wa dhahabu wapaa Barrick North Mara


Rais wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow.

Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
-------------------------------------------

UZALISHAJI wa dhahabu katika mgodi wa North Mara umeongezeka, huku utafiti ukionesha uwezekano wa mgodi huo kuendelea kuwa na masisha marefu zaidi, Rais wa Kampuni ya Barrick, Mark Bristow amesema.

Aidha, Bristow amesema Barrick imeshuhudia ongezeko la uzalishaji wa madini hayo katika mgodi wake mwingine wa Bulyanhulu uliopo mkoani Shinyanga.

Migodi ya North Mara na Bulyanhulu inaendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals, tangu mwaka 2019.

Akizungumza na vyombo vya habari katika Shule ya Sekondari ya Ingwe iliyopo Nyamongo, kilomita chache kutoka mgodi wa North Mara wilayani Tarime juzi, Bristow alisema tani 505,000 za madini na udongo usiotakiwa zilichimbwa mgodini katika kipindi cha robo mwaka kilichopita [Julai 1 hadi Septemba 30, 2022].

Alitaja uboreshaji wa shughuli za uchimbaji katika migodi hiyo, umahiri wa wafanyakazi wake, ushirikiano wa Barrick, Serikali na Kampuni ya Twiga Minerals kama baadhi ya mambo makubwa yaliyochangia mafanikio hayo.

Habari njema ni kwamba Kampuni ya Barrick imewekeza shilingi zaidi ya trilioni tano katika uchumi wa Tanzania tangu ichukue migodi ya North Mara na Bulyanhulu mwaka 2019 na kuifanya kuwa moja wa vinara wa kuchangia ukuaji wa uchumi nchini kwa sasa.

“Barrick ni mchangiaji mkubwa wa uchumi na asilimia 96 ya wafanyakazi wetu ni Watanzaia,” alisema Bristow ambaye pia ni Afisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa Barrick.

Kwa mujibu wa Bristow, kati ya asilimia 96 ya wafanyakazi Watanzania walioajiriwa na Barrick, asilimiaa 45 wanatoka katika jamii zinazozunguka migodi hiyo, na kwamba asilimia 58 ya wafanyakazi wanashikilia nafasi za juu migodini.

Aidha, alisema katika kipindi cha robo mwaka kilichopita, migodi ya North Mara na Bulyanhulu ilitumia dola za Kimarekani milioni 339 kulipa zabuni na watoa huduma wa Kitanzania.

Bristow alisema mbali na uzalishaji wa madini kuongezeka katika migodi ya North Mara na Bulyanhulu, utafiti pia umeonesha mafanikio kuhusu uwezekano wa kampuni hiyo kupanua shughuli za uchimbaji.

Alifafanua kuwa wakati migodi ya North Mara na Bulyanhulu ikiwa imejipang kufikia uzalishaji wa pamoja wa wakia zidi ya 500,000 kwa mwaka wa pili mfululizo, Kampuni ya Barrick inatarajia kupanua shughuli zake Afrika Mashariki.

“Tunaendelea kulenga ukuaji zaidi kupitia uchunguzi na kujumuisha leseni muhimu. Fursa za upanuzi zinatathminiwa katika maeneo ya Gokona na katika eneo zaidi la Bulyanhulu.


Matokeo ya uchimbaji wa chini ya ardhi katika eneo la Gokona yanaonesha kuongeza muda wa maisha ya mgodi wa North Mara,” Bristow alisema katika mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na viongozi wa kijamii kutoka vijii vinavyozunguka mgodi wa North Mara.

Alisema kampuni hiyo ina mwelekeo chanya kuhusu upanuzi wa rasilimali katika migodi yake hiyo miwili.

“Uelewa mzuri zaidi wa usanifu wa ikolojia tulio nao katika ukanda huu utaongeza uwezo wetu wa kugundua fursa mpya za maendeleo za daraja la kimataifa katika maeneo tuliyo na maslahi nayo,” alisema Rais huyo wa Barrick.

Bristow ambaye alidokeza kuwa siku hiyo hiyo alikuwa amepata fursa ya kukutana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na kuzungumzia ushirikiano kati ya Barrick na Kampuni ya Twiga Menerals na maendeleo ya sekta ya elimu, alisisitiza kuwa Barrick itaendelea kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Seikali ya kuendeleza sekta hiyo nchini.

Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Barrick Tanzania, Dkt Melkiory Ngido alisema hakuna tukio lolote baya la kimazingira au usalama ambalo limeripotiwa katika migodi ya Barrick tangu Januari hadi kipindi cha robo ya tatu kilichopita.

“Rekodi yetu katika masuala ya usalama na mazingira ni ya hali ya juu,” alisema Dkt Ngido.

Kuhusu uwekezaji katika maendeleo ya jamii, Dkt Ngido alisema Kampuni ya Barrick imetoa Sh bilioni 17 kupitia Mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) huku maeneo ya elimu, maji, afya, uchumi na usalama wa chakula yakipewa kipaumbele katika vijiji vilivyo jirani na migodi ya North Mara na Bulyanhulu.

Alitolea mfano uanzishaji wa shamba darasa ambalo litawezesha vijana 100 kiuchumi katika kijiji cha Matongo kilichopo jirani na mgodi wa North Mara.


Katika hatua nyigine, Dkt Ngido alisema eneo la uliokuwa Mgodi wa Dhahabu Buzwagi linabadilishwa kuwa eneo maalumu la uwekezaji.

“Soko la kwanza la kwanza la mazao ya hawa vijana ni mgodi na tupo tayari kuwa- support,” alisema Dkt Ngido.

Kabla ya mkutano huo kuhitimishwa, Rais wa Barrick, Bristow, alikabidhi hundi nne za dola 40,000 zilizotolewa msaada na kampuni hiyo kwa ajili ya kuchangia gharama za elimu kwa watoto wanaotoka mazingira magumu.


Viongozi wengine waliohudhuria mkutano huo ni pamoja na Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dkt Yahya Nawanda, Mkuu wa Wilaya ya Tarime Kanali Michael Mntenjele na Mbunge wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara.

Chanzo: Sauti ya Mara

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages