NEWS

Monday 5 December 2022

Muderspach yang’ara matokeo ya darasa la saba, wanafunzi 59 wapiga A, wamo wasichana 26Na Mwandishi Wetu, Tarime
----------------------------------------------

WANAFUNZI 59 wa Muderspach Primary School wamepata ufaulu wa daraja A na kuwa miongoni mwa shule zilizofanya vizuri katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kuhitimu Darasa la Saba mwaka 2022, yaliyotangazwa na Baraza la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA), wiki iliyopita.

“Tunamshukuru Mungu wanafunzi wetu wamefaulu vizuri - ambapo 59 wamepata daraja A na 11 wamepata ufaulu wa daraja B,” Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Paul Basondole aliiambia Sauti ya Mara kwa njia ya simu, jana.

Mwalimu Basondole alisema kati ya wanafunzi 59 waliopata ufaulu wa daraja A, 26 ni wasichana na 33 ni wavulana.

“Kwa upande wa waliopata daraja B, wasichana ni watano na wavula ni sita. Jumla ya wanafunzi wetu waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi shuleni kwetu walikuwa 70,” alifafanua.

Alitoa wito kwa wazazi kuendelea kuiamini shule hiyo ya Muderspach, akisema imejipanga kuendelea kuwaandaa vizuri wanafunzi kiroho, kimwili, kiakili na kijamii.

Pia shule hiyo, Mwalimu Basondole alisema imefanikiwa kuwa na upekee wa kuwa na huduma ya maji safi na salama kwa wanafunzi wake saa 24.

“Tuna maji safi na salama kwa wanafunzi wetu na huu pia ni upekee wa shule yetu ya Muderspach,” alisema.

Muderspach ni shule inayomilikiwa na Waadventista Wasabato Jimbo la Mara. Ipo katika eneo la Kibumaye, takriban kilomIta tano kutoka mjini Tarime, mkoani Mara.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages