NEWS

Friday 30 December 2022

Shirika la Stories Sweden lapeleka umeme jua vijijini


Mfadhili kutoka shirika la Stories Sweden akisaidia kuweka taa za sola kwenye mojawapo ya nyumba katika kijiji cha Ngarenanyuki wilayani Arumeru

Na Marycelina Masha
---------------------------------

SHIRIKA lisilotengeza faida lijulikanalo kama Stories Sweden, linatoa nishati endelevu ya jua (sola) bure katika maeneo ya vijijini barani Afrika.

Shirika hilo limeamua kuongeza kasi ya upatikanaji wa umeme kwa familia nyingi zaidi iwezekanavyo, ili kuwafikia watu waishio katika maeneo yaliyo nje ya gridi za taifa.

Likiwa limeanzishwa mwaka 2022 na Douglas Solberg, shirika hilo la Kiswidi limefadhili na kuunganisha umeme wa jua kwa ajili ya taa na kuchaji simu kwa familia 30 nchini Tanzania.

Familia ambazo tayari zimenufaika na mradi huo ni wakazi wa vijiji vya Olkung’wado, Mwakey, Kwa Loki na Lendoiya katika wilaya ya Arumeru mkoani Arusha.

“Kwenye tovuti yetu ijulikanayo kama storiessweden.org, wafadhili huchangia miradi kwa pamoja, na kupata taarifa muhimu kila mara ili wajue matokeo ya michango yao. Hii inawahakikishia uwazi. Tunapenda kuwashirikisha wafadhili wetu mara nyingi iwezekanavyo,” anasema Solberg.

Nchini Tanzania, shirika hili limeshirikiana na shirika jingine la Africa Amini Alama, ambao ndio waliosaidia katika ufungaji wa paneli za nishati ya jua.

Wakionesha furaha kubwa baada ya paneli za jua kufungwa, wanavijiji hao walishukuru shirika hilo la Sweden kwa kuboresha maisha yao ya kila siku, na kuongeza kwamba hawakutarajia kamwe kuona taa za umeme majumbani mwao. Lakini sasa jambo hilo limewezekana.

“Mungu awabariki wote,” anasema mmoja wa wanavijiji hao.

Mama na mtoto wake wakifurahia baada ya kuwasha taa ya sola katika kijiji cha Kwa Loki wilayani Arumeru, ikiwa ni ufadhili kutoka shirika la Stories Sweden

Salome Kitolomai, ambaye watoto wake wanasoma kijijini humo, anasema ana furaha kubwa kwani wataweza kujisomea wenyewe saa za jioni na kufanya kazi za shuleni kwa vile sasa nyumba yake inang’ara kutokana na umeme.

Anatoa ombi kwa shirika la Stories Sweden kuongeza zaidi umeme wa jua ili kukifanya kijiji kuwa mfano, katika mipango yao ya siku za usoni.

“Tunayo bahati ya kuwa watu wa kwanza kupata nishati ya jua bure. Tunawashukuru sana wafadhili wetu,” anasema Salome kutoka kijiji cha Olkung’wado.

Shirika hilo lina mpango wa kutekeleza mradi huo katika awamu nyingine mbili, kutegemeana na upatikanaji wa fedha.

“Mwanzoni mwa 2023, Shirika la Stories Sweden limepanga kufunga mfumo kamili wa nishati ya jua katika shule tatu pamoja na kituo cha kulea watoto yatima kwa gharama ya dola za kimarekani 70,000. Katika awamu ya tatu, tunatarajia kujenga gridi-ndogo katika vijiji vilivyoko nje ya gridi ya taifa. Lengo letu ni kupatia kila familia umeme,” anasema Solberg.

Nchini Tanzania, maeneo ya vijijini ambapo wananchi wengi huishi, yanapata huduma ya umeme kutoka kwa Wakala wa Serikali wa Umeme Vijijini kwa kuunganishwa kwenye gridi ya taifa.

Hata hivyo, maeneo ya pembezoni yanapata kiasi kidogo cha nishati hii kutokana na changamoto ya ufikiwaji, barabara na watu wenyewe kujenga maeneo yaliyo mbali mbali, kutokana na mahitaji ya shughuli zao nyingi zikiwemo kilimo na ufugaji.

Vile vile kuna uhitaji mkubwa wa umeme katika zahanati na vituo vya afya, ambako dawa na chanjo zipo katika hatari ya kuharibika kutokana na ukosefu wa umeme na vifaa vya kisasa vya kuhifadhia.

Kwa sasa, zipo zahanati ambazo hutumia taa za mafuta lakini hizi zina changamoto ya uharibifu wa mazingira na siyo endelevu. Pia wakati mwingine mafuta ya taa ni adimu. Shughuli za huduma ya afya zinaweza kuendeshwa nyakati zote hata usiku, iwapo umeme wa uhakika utakuwepo.

Shirika hili la Kiswidi kwa sasa linatafuta wabia na michango ili kuendeleza huduma hii ya nishati ya jua. Kama una nia, unakaribishwa kutembelea tovuti yao ya storiessweden.org ili upate habari zao zaidi na jinsi ya kujiunga ukiwa kama mfadhili au mwenye kutaka kufadhiliwa.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages