NEWS

Monday 30 January 2023

Wassira asimulia usiyoyajua kuhusu Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere Butiama


Stephen Wassira

Na Mwandishi Wetu
---------------------------------

MWANASIASA nguli na kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wassira amepongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuonesha juhudi za kutimiza ndoto ya kujenga Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia (MJNUAT) katika wilaya ya Butiama mkoani Mara.

Katika mahojiano maalumu na wahariri wa Sauti ya Mara kwa njia ya simu juzi, Wassira alisema mpango wa Serikali ya Awamu ya Sita wa kukwamua chuo hicho umepewa umuhimu unaostahili.

“Serikali imechangamkia hicho chuo, imepata fedha na inataka kujenga majengo ya kisasa. Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa ameelewa na amechukua initiative (hatua).

“Tunaomba juhudu ambazo zinafanywa na serikali ziharakishwe na mawazo yaliyotolewa huko nyuma yatiliwe maanani,” Wassira ambaye kwa sasa ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anasema katika mahojiano hayo.

Anaona kuwa chuo kikuu hicho kitasaidia kuchangamsha maisha na uchumi wa wananchi wa Butiama, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.

“Butiama yenyewe ni Butiama ya Mwalimu na sisi wote tungependa kuona Butiama iliyochangamka, na actually (kiukweli) hiyo ndio ilisababisha tukafanya Butiama ikawa wilaya kwa kuweka taasisi za kudumu kule. Taasisi nyingine ni chuo kikuu hicho,” anasema Wassira.

Anaongeza kuwa chuo hicho kikiwa na maelfu ya wanafunzi, Butiama itachangamka kiuchumi, lakini pia kitasaidia kuleta mageuzi ya kilimo katika mkoa wa Mara.

“Kwa kuwa ni chuo cha kilimo, na Mara ni mkoa wa kilimo, tafiti zitakazofanyika pale zitasaidia kufanya kilimo kuwa cha kisasa zaidi katika mkoa wa Mara,” anasema.

Mtazamo mwingine wa Wassira ni kwamba matokea ya tafiti hizo pia yatasaidia kuongeza uzalishaji wa mazao ya kilimo na kupunguzia wananchi umaskini.

Wassira anaweka wazi kuwa yeye na aliyewahi kuwa Mbunge wa Butima, Nimrod Mkono, walihusishwa kutoa maoni ya kuanzishwa kwa chuo kikuu hicho wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne.

“Sisi tulishirikishwa kutoa maoni, nakumbuka mimi nilihojiwa pamoja na Nimrod Mkono wakati tukiwa wabunge wa mkoa wa Mara,” anasema Wassira ambaye aliwahi kuwa Mbunge wa Bunda na kuhudumu kama waziri kwenye wizara mbalimbali nchini, ikiwemo ya kilimo.

Kwa mujibu wa kada huyo wa chama tawala - CCM, katika maoni yao walishauri chuo hicho kiwe cha kilimo na sayansi kwa ujumla, makao yake yawe Butiama na kiwe na vitivo katika wilaya mbalimbali.

Mfano anasema moja ya maoni yao ni chuo hicho kuwa na kitivo cha utafiti wa kilimo katika wilaya ya Tarime, kitivo cha uvuzi katika wilaya ya Rorya na kitivo cha utalii katika wilaya ya Serengeti.

“Tulipendekeza pia kuwa Chuo cha Ualimu Bunda kiwe pia ni sehemu ya kitivo cha chuo kikuu hicho na kifundishe walimu wa sayansi,” anaongeza Wassira na kubainisha kuwa uamuzi wa kuanzisha chuo hicho ulianza mwaka 2010 wakati wa Serikali ya Awamu ya Nne chini ya Rais Dkt Jakaya Kikwete.

Anadokeza kuwa pia Hospitali ya Kwangwa iliyopo wilaya ya Musoma ilipendekezwa kuwa sehemu ya kitivo cha Chuo Kikuu cha Mwalimu Julius Nyerere cha Kilimo na Teknolojia.

Wassira anasema haoni tatizo kuhusu taarifa zinazotolewa kuwa chuo hicho kimekaa muda mrefu bila kusajili wanafunzi, huku kikiwa kwenye majengo ya muda wakati ujenzi wa majengo yake ukisubiriwa.

“Wanafunzi huwa wanakuwa allocated (hupangiwa sehemu ya kwenda) na Wizara ya Elimu, sasa kama hakuna selection (uteuzi) iliyofanyika wasingeenda.

“Ninachojua ni kwamba kile chuo kilichelewa kupata wanafunzi kwa sababu mchakato wa kuhamisha majengo na mchakato wa wizara kupeleka wanafunzi ulikuwa haujakamilika,” anasema Wassira.

Aidha, anasema pia hakuna tatizo la wafanyakazi wakiwemo maprofesa waliopelekwa katika chuo hicho kuendelea kulipwa mishahara yao kama kawaida kwani wamekuwa wakifanya kazi nyingine, ikiwemo kufanya mawasiliano na Wizara ya Elimu kuhusu mchakato wa uanzishaji wa chuo hicho.

“Kile chuo ilibidi kianzishwe mahali ambapo kuna majengo, hivyo kikaanzishwa kwa majengo ya sekondari pale Busegwa,” anabainisha Wassira.

Hivi karibuni, Kamati ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii ilitembelea chuo hicho na kubaini kuwa hakijawahi kusajili mwanafunzi tangu mwaka 2010 kilipoanzisha, licha ya kuwa na wafanyakazi akiwemo Makamu Mkuu wa Chuo na wahadhiri kadhaa ambao wanalipwa msharaha kutoka serikalini.

Lakini Wassira pamoja na kukiri kuwa ujenzi wa chuo hicho umechelewa, anasema muda uliopita tangu kuanzishwa kwa chuo hicho haufiki miaka 13 kama ambavyo imeripotiwa. “Tukubali kuwa tumechelewa lakini sasa serikali imeamua kukijenga,” anasema.

Gazeti hili lilimtafuta pia Chifu wa Kabila la Wazanaki, Japhet Wanzagi kutoa maoni yake ambapo aliipongeza serikali kwa kutoa mabilioni ya fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho, lakini akataka kianze kusajili wanafunzi.

“Serikali imetoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa chuo, ni jambo zuri na nimesikia kuwa Oktoba mwaka huu kitaanza kusajili wanafunzi, litakuwa jambo zuri,” anasema Chifu Wanzagi.

Chanzo: SAUTI YA MARA

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages