Na Mara Online News
-------------------------------------
MKUU wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (pichani), amekagua uondoaji wa maboma ya watu waliolipwa fidia katika eneo la Komarera kwa ajili ya kupisha upanuzi wa shughuli za Mgodi wa Dhahabu wa North Mara.
Mgodi huo unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
“Nimekuja hapa Komarera kutembelea zoezi linaloendelea la kuwaondoa watu waliokwishalipwa fidia baada ya tathmini iliyofanywa na Serikali,” DC Mntenjele ameiambia Mara Online News muda mfupi baada ya kutembelea eneo hilo leo Jnuari 4, 2023.
Amewataka watu wote waliokwishachukua malipo ya fidia za mali zao kuondoka ili kutokwamisha mgodi wa North Mara kupanua shughuli zake za uchimbaji madini.
“Kuna watu wamekwishachukua fedha za fidia lakini bado wanaendelea kuwepo katika eneo hili, maana yake wanakwamisha mgodi kuendeleza uwekezaji katika eneo hili.
“Nilikwishasema tokea awali kwamba maadamu walishalipwa, basi waondoke kama ambavyo makubaliano yalikuwa, ili kupisha mgodi ufanye maendeleo ambayo unakusudia kuyafanya.
“Lakini kwa wale ambao hawajachukua hela zao - maana bado hela nyingine zipo mgodini, waende wakachukue,” amesisitiza Mkuu huyo wa wilaya.
No comments:
Post a Comment