NEWS

Sunday 29 January 2023

Matokeo kidato cha nne hadharani, 333 wafutiwa wakiwemo walioandika matusi, NECTA yasitisha utaratibu wa kutangaza shule, wanafunzi boraNa Mwandishi Wetu
---------------------------------

BARAZA la Taifa la Mitihani Tanzania (NECTA) limesitisha utaratibu liliokuwa nao wa kutangaza shule na wanafunzi bora wa matokeo ya kidato cha nne.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini D res Salaam leo Januari 29, 2023, Kaimu Katibu Mtendaji wa NECTA, Athumani Amasi (pichani), amesema Baraza hilo limebaini kuwa utaratibu huo ulikuwa unazitangazia biashara baadhi ya shule.

Amasi ameyasema hayo wakati akitangaza matokeo ya Mitihani ya Taifa ya Kidato cha Nne (CSEE) na Maarifa (QT) iliyofanyika Novemba 14 hadi Desemba 1, 2022, Tanzania Bara na Visiwani.

"Kutangaza shule ya kwanza huenda tulikuwa tunakufanyia Marketing kwa kuitaja tu hiyo shule, shule zipo nyingi zaidi ya elfu 18, sasa unapotaja moja sidhani kama ina tija," amesema Athumani Salumu.

Amesema kumtangaza mwanafunzi bora wa mtihani huo hakuna tija katika hilo kwani hauwezi kumtangaza mwanafunzi mmoja kati ya wanafunzi wote Tanzania ambao huenda pia mazingira yao ya kusoma yalikuwa tofauti.

"Unamtaja mtu kwamba ameongoza katika kundi ambalo pamoja na kwamba wamefanya mtihani huo huo lakini hawakusoma katika mazingira yanayofanana, alafu sasa unampa sifa mtu mmoja," amesema Amasi.

Kuhusu matokeo ya mitihani, amesema NECTA imefuta ya wanafunzi 333 akiwemo mmoja wa Maarifa kwa kufanya udanganyifu.

Amasi amsema watahiniwa wengine wanne wamefutiwa matokeo kutokana na kuandika matusi katika mitihani yao.

Kwa mujibu wa Amasi, vituo vitatu vimefungiwa kufanya mitihani baada ya kuthibitika kupanga na kufanya udanganyifu.

Katika matokeo hayo, amesema kati ya watahiniwa 520,558 waliofanya mtihani, 456,975 sawa na asilimia 87.79 wamefaulu kwa kupata daraja la kwanza hadi la nne.

Amesema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 0.49 ukilinganisha wa mwaka 2021, ambapo watahiniwa 422,388 sawa na asilimia 87.30 walifaulu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages