NEWS

Tuesday 28 February 2023

Ng’ong’a akabidhi msaada wa mahindi akihamasisha wazazi kuchangia chakula cha wanafunzi Rorya



Na Mara Online News
-----------------------------------

MWENYEKITI wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Gerald Ng'ong'a (katikati pichani juu), ametoa msaada wa mahindi magunia 10 kuchangia chakula cha wanafunzi katika shule za msingi na sekondari za katwa wilayani humo.

Sambamba na msaada huo, Ng’onga amejitolea kulipa gharama za wapishi - kiasi cha shilingi 50,000 kwa miezi mitatu ya Machi, Aprili na Mei 2023, kwa kila shule iliyoanza kutekeleza mpango huo.

Ng’ong’a ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Rabuor kwa tiketi ya chama tawala - CCM, alikabidhi msaada huo katani hapo jana wakati wa mkutano wake wa kuhamasisha wazazi n walezi kuchangia chakula cha wanafunzi wawapo shuleni, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuinua kiwango cha taaluma katika shule za msingi na sekondari za kutwa wilayani Rorya.

“Shughuli hii tunaitekeleza kwa maslahi mapana ya watoto wetu na kwa faida yetu sisi wenyewe. Saula la chakula shuleni ni muhimu na ni ajenda ya taifa. Viongozi wameshaona mbele kwamba tusipofanya hivyo leo, kesho ni shida.

“Kwa hiyo ni jukumu letu sisi viongozi wa chini ni kutekelez melekezo ya viongozi wetu wa juu. Rais ameingia mkataba na viongozi kuhakikisha kwamba suala la lishe nchi nzima ni ajenda kwa kila kijiji, kila kitongoji, kila shule, kila sehemu ndani ya Tanzania, siyo Rorya peke yake,” alisema Ng’ong’a.

Mwenyekiti Ng'ong'a (katikati) akikabidhi msaada wa mahindi

Mwenyekiti huyo wa halmashauri alisema serikali imefuta ada katika shule za msingi na sekondari ili kuwapunguzia wazazi na walezi mzigo wa gharama za mahitaji kwa wanafunzi.

“Serikali kadiri inavyozidi kutoa nafuu kwenye michango ya shule/ elimu ndivyo wazazi wanapata nafuu ya kufanya mambo mengine. Elimu ya msingi hakuna ada, sekondari kidato cha kwanza mpaka cha sita hakuna ada, zile hela ambazo tungelipa ada tuzielekeze kwa matumizi ya watoto wetu na mahitaji mengine, faida yake ni kubwa sana.

“Mafanikio ya watoto wetu leo yanategemea afya ya akili na huduma ya chakula, wanaposhinda njaa muda mrefu wakienda kwenye mtihani kufikiri na kufanya vizuri kunakuwa kudogo sana

“Programu ya chakula inasaidia sana kufanya vizuri kufaulu, kujenga maarifa, hivyo shughuli hii lazima iendelee na mimi niko pamoja nanyi, shule zote zilizoanza na mimi leo ninazipa mahindi kila moja gunia moja,” Ng’ong’a alisisitiza.

Kwa upande mwingine Ng’ong'a amekabidhi msaada wa mabati kadhaa kwa ajili ya ujenzi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) Rabuor.

Mwenyekiti Ng'ong'a (katikati) akijumuika na wananchi kucheza muziki

Ng’ong’a alishuhudia mapokezi makubwa kutoka kwa wananchi wa rika tofauti, huku wakionesha kufurahia juhudi zinazofanywa na kiongozi huyo katika kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika wilaya hiyo - ambayo kwa sehemu kubwa inapakana na Ziwa Victoria, Kaskazini mwa mkoa wa Mara.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages