NEWS

Wednesday 29 March 2023

CCM yawataka wananchi Nyanungu kuwa watulivu, yamjibu Diwani Tiboche, yakemea viongozi wanaosusia vikao vya suluhuNa Mara Online News
------------------------------------

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime kimewataka wananchi wa kata ya Nyanungu kuendelea kuwa watulivu kipindi hiki cha uwekaji wa vigingi vya mpaka wa vijiji vyao na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, huku kikiwatia moyo kuwa Serikali ya chama hicho iko makini kuhakisha maslahi yao yanazingatiwa.

“CCM ndicho chama pekee kinachowatetea wanyonge, hakuna mwananchi atakayelia, hakuna mwananchi atakayepata taabu, na mwisho wetu utakuwa mzuri sana,” amesema Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Valentine Maganga (pichani juu) katika mazungumzo na Mara Online News ofisini kwake leo mchana.

Kuhusu kauli iliyotolewa na Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard - ya kutishia kujiuzulu kwa kile anachodai ni kutokubaliana na uwekaji wa vigingi hivyo, Maganga amesema hayo ni maoni binafsi ya diwani huyo.

“Akiona mawazo yale ni vizuri yapate ufumbuzi, ni vizuri kuyaleta kupitia njia sahihi. Siyo vizuri kutumia mitandao wakati njia sahihi unaijua,” Maganga amesema na kuongeza kuwa mwazo ya kujiuzulu ni ya diwani huyo binafsi, siyo ya CCM.

Jana, Diwani Tiboche ambaye anatokana na chama hicho tawala alikaririwa kwenye mitandao ya kijamii akitishia kujiuzulu wadhifa huo.

Aidha, Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Tarime amewataka viongozi wa serikali za vijiji husika ambavyo ni Kegonga na Nyandage kutokubali kugomeshwa na wanasiasa kujitokeza kushiriki vikao vikiwemo vinavyoitishwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee kwa ajili ya utatuzi wa mgogoro uliopo.

“Tabia ya kususia vikao waache, suluhisho lolote linapatikana kwenye vikao, waache siyo tabia nzuri,” amesema Maganga na kusisitiza kuwa tabia hiyo ya kukwepa vikao haitasaidia kutatua mgogoro huo.

Kwa upande mwingine, Maganga ameeleza kushangazwa na kitendo cha viongozi wa wananchi wa maeneo hayo kukwepa kukutana na viongozi wateule wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wanaokwenda kusuluhisha mgogoro huo.

“Unamkwepa mkuu wako wa wilaya, unamkwepa mkuu wako wa mkoa, na hao ndio wameteuliwa na Mheshimiwa Rais kusimamia mambo yote ya Serikali ngazi ya wilaya na mkoa, unaenda kwenda vyombo vya habari haitusaidii,” Maganga amesisitiza.

Ametumia nafasi hiyo pia kuwakemea wanasiasa wanaopotosha umma kuhusu suala la uwekaji wa vigingi vya mpaka wa wanavijiji na Hifadhi ya Serengeti, huku akiwataka wananchi wa maeneo hayo kukataa ‘swaga’ zao kwa kuwa wanatumia mgogoro uliopo kutafuta umaarufu na maslahi yao binafsi.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages