NEWS

Tuesday 7 March 2023

Kituo cha Afya Bumera mbioni kuanza kutoa huduma kwa wananchi Tarime Vijijini


Jengo la Kitengo cha Wagonjwa wa Nje (OPD) la Kituo cha Afya Bumera

Na Mugini Jacob
------------------------

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Tarime (Vijijini), Solomon Shati amesema atalazimika kusimamia mwenyewe ukamilishaji wa baadhi ya majengo katika kituo kipya cha afya Bumera, ambacho huduma zake zinasubiriwa na mamia ya wananchi kwa shauku kubwa.

Nguvu kubwa kwa sasa itaelekezwa katika kukamilisha uezekaji na umaliziaji wa jengo la huduma za upasuaji, mama na mtoto, huku ujenzi wa jengo la kufulia ukiendelea katika mradi huo wa afya.

“Kuanzia wiki ijayo [wiki hii] nitahamia pale (eneo la mradi wa ujenzi wa kituo cha afya Bumera) ili kazi iishe, kituo kianze kutoa huduma za matibabu kwa wananchi,” DED Shati aliiambia Sauti ya Mara wiki iliyopita, baada Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime kupita na kukagua maendeleo ya ujenzi wa kituo hicho na kutoa maelekezo kadhaa.

Baadhi ya maelekezo yaliyotolewa na kamati hiyo ambayo iliongozwa na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho, ni ukamilishaji wa uezekaji wa jengo la huduma za upasuaji, mama na mtoto ndani ya siku tatu.

“OPD (Kitengo cha Wagonjwa wa Nje) na maabara zipo tayari na baada ya wiki mbili huduma zitanaza kutolewa kwa wananchi,” alisema Mkurugenzi huyo.

Mkurugenzi Solomon Shati

Serikali ya Awamu ya Sita imetoa shilingi milioni 500 kugharimia ujenzi wa kituo hicho kutokana na makusanyo ya fedha za tozo.

Shati alisema fedha hizo zilishatolewa kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho, huku kamati za ujenzi na mapokezi zikipata mafunzo ya usimamizi.

Hata hivyo Mkurugenzi huyo alidokeza mbele ya wajumbe wa Kamati ya Siasa kuwa hatua mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kumweka pembeni mtumishi anayetajwa kwenye ripoti ya uchunguzi iliyobaini dosari kadhaa katika mradi huo, ili kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.

Wananchi wa kata ya Bumera wanasema ujenzi wa kituo hicho utakuwa mkombozi kwao, huku wasiburi huduma hizo kwa shauku kubwa.

“Tunaomba kituo kianze kutoa huduma, wananchi wanapata shida, hasa wazazi,” James Nokwe, mmoja wa wananchi wa kata hiyo ya Bumera aliwambia wajube wa kamati hiyo ya siasa ya chama tawala.

Kwa sasa wananchi wa kata hiyo wanalazimika kutembea au kusafiri umbali mrefu kwenye kutafuta huduma za matibabu, hivyo kukamilika kwa kituo hicho kutaleta ahueni kubwa kwao.

“Kwa kweli hiki kituo cha afya kitatutoa gizani, wagonjwa wanapata shida na tunaishukuru Serikali yetu maana sasa tutapata huduma za matibabu jirani bila kutembea umbali mrefu,” alisema mkazi mwingine wa kata hiyo, Thomas Keraryo.

Ujenzi wa Kituo cha Afya Bumera unatarajia kupunguza vifo vya mama na mtoto katika kata hiyo.

Kituo hicho kinatarajiwa kutoa huduma za matibabu kwa wananci zaidi ya 4,000 kwenye vijiji vinane vya kata hiyo; ambavyo ni Turugeti, Kwisarara, Kitenga na Kiterere.

Wakati huo huo, Kamati ya Siasa ya CCM Wilaya ya Tarime imeelezwa kuridhishwa na utekelezaji wa miradi iliyoikagua katika Halmashauri hiyo ya Tarime (Vijijini).

Baadhi ya miradi hiyo ni Shule ya Sekondari mpya ya Bukira ambayo tayari imepokea wanafunzi wa kidato cha kwanza mwaka huu [2023] baada ya ujenzi wake kukamilika kwa gharama ya shilingi milioni 470 zilizotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita, ikiwa ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muunagno wa Tanzania, Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

Mradi mwingine ambao utekelezaji wake ulipongezwa na kamati hiyo ni ujenzi wa chumba cha darasa uliotengewa shilingi milioni 20 za mapato ya ndani ya halmashauri, ambao umekamilika na chenji ya shilingi laki tatu kubaki.

“Kamati ya Saisa tumekagua hili darasa lililojengwa kwa mapato ya ndani, tumeridhika na kazi nzuri iliyofanyika,” alisema Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Ngicho.

Chanzo: SAUTI YA MARA

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages