NEWS

Tuesday, 7 March 2023

Maadhimisho Siku ya Wanawake Duniani yafana Tarime, Barrick North Mara washiriki



Na Mara Online News
------------------------------------

MBUNGE wa Jimbo la Tarime Vijijini, Mwita Waitara ameushukuru na kuupongeza Mgodi wa Dhahabu wa North Mara kwa kuvipa vikundi vya wanawake wajasiriamali fursa ya kupeleka huduma mbalimbali katika mgodi huo, unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Waitara alitoa shukrani na pongezi hizo wakati akihutubia mamia ya wananchi katika maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani, yaliyofanyika kiwilaya jana Machi 6, 2023 kwenye viwanja vya Shule ya Sekondari Ingwe iliyopo Nyamongo, kilomita chache kutoka mgodini hapo.

“Mwanzoni kulikuwa na shida, na akina mama wa hapa wanajua, siku wanafanya Family Day [Barrick North Mara Family Day 2022] nilikuwepo, waliniambia akina mama wengi wanatoa huduma, vikundi mbalimbali vinahudumia kwenye mgodi. Hapo kabla havikuwepo.

“Akina mama wakiwezeshwa wanaweza, fedha zao nyingi zinatumika kwenye familia, akina baba wengi sisi fedha zetu nyingi zinakuwa na maswali mengi,” Waitara alisema.
Mbunge Waitara (kulia) akizungumza katika maadhimisho hayo

Mbunge Waitara pia aliwashukuru na kuwapongeza wakandarasi wanaofanya kazi na mgodi wa North Mara, ambao mapema jana walianza maadhimisho hayo kwa kutembelea na kutoa misaada mbalimbali kwa wagonjwa katika Kituo cha Afya Nyangoto, jirani na viwanja hivyo.

“Nimefurahi kwamba wale wadau wa maendeleo wameanzia Kituo cha Afya Nyangoto na nimewahi kufanya ziara pale tukiwa na viongozi wa chama na serikali, dakitari akaonesha changamoto zilizokuwepo. Wale wadau wamepunguza changamoto tuliyoikuta siku ile, wamepeleka vifaa vyenye thamani ya shilingi milioni 25.

“Lakini bahati nzuri msaada wao ulilenga kusaidia mama na mtoto, wametembelea wagonjwa waliolazwa na wamefarijika sana. Wengine wamepata sabuni, wengine vitenge, wengine juisi, tuendelee kushikana mikono,” alisema mbunge huyo wa Tarime Vijijini.

Kwa upande mwingine, Mbunge Waitara alitoa wito wa kuziomba taasisi za umma katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuangalia uwezekano wa kununua na kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na kuuzwa na vikundi vya wanawake ili kuwainua kiuchumi.

“Akina mama wanalima nyanya, vitunguu, wanafuga kuku, wanauza mayai, sabuni za chooni, waungeni mkono kwa kununua bidhaa kwao ili wapate hela na kuzalisha kwa tija. Kama kutakuwa na mapungufu ya quality (ubora) tuna wataalamu - wawashauri wazalishe vitu vinvyokubalika,” Waitara alisisitiza.

Aliongeza kuwa wanawake wanastahili kupewa kipaumbele pia katika utoaji wa mikopo inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, kwa kuwa ni wengi wao waminifu na wamekuwa wakiitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.

“Tumepofutilia hii mikopo ya asilimia 10, takwimu zinaonesha wanawake wanaipeleka kwenye malengo yaliyokusudiwa, na pili ni waminifu na marejesho yao ni mazuri,” Waitara alisema.

Kuhusu elimu, Mbunge Waitara aliitoa wito kwa jamii kuhakikisha mtoto wa kike anapata elimu bora. “Elimu itawasaidia watoto wa kike na wanawake kujitambua, kuwa wajasiriamali wazuri, wataajiriwa, watajiajiri, na shida nyingi katika familia zitapungua kwa sababu wengi watakuwa na uwezo wa kujisimamia na kushika nafasi mbalimbali,” alisisitiza.

Katika maadhimisho hayo, wafanyakazi wa mgodi wa Barrick North Mara wakiwemo wanawake, waliongozwa na Meneja Mahusiano wa mgodi huo, Francis Uhadi.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages