Na Mara Online News
---------------------------------
MGODI wa Dhahabu wa North Mara umetumia shilingi takriban milioni 40 kugharimia ukarabati mkubwa wa gari la kubeba wagonjwa (ambulance) la Kituo cha Afya Nyangoto kinachotoa huduma kwa maelfu ya wakazi wa vijiji vilivyo jirani na mgodi huo.
Viongozi mbalimbali wa kijamii na serikali kutoka kata ya Matongo na vijiji vya Mjini Kati na Nyangoto wamejitokeza mapema leo asuhubi kupokea gari hilo kituoni hapo baada ya ukarabati wake kukamilika.
Viongozi hao akiwemo Diwani wa kata ya Matongo, Godfrey Kegoye na Diwani wa Viti Maalumu, Felista Range wameshukuru mgodi huo kwa kukubali na kufanyia kazi ombi lao la kukarabati gari hilo baada ya kuwa limechakaa.
Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.
“Mungu amesikia kilio chetu na nipende kuwashukuru Barrick kwa mliochokionesha,” amesema Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Mjini Kati, Paul Bageni wakati wa mapokezii wa gari hilo.
Kwa mujibu wa Bageni, kituo hicho cha serikali kilichopo chini ya Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, kinahudumia idadi kubwa ya wananchi wa maeneo ya Nyamongo hadi wilaya jirani ya Serengeti.
Diwani Kegoye ambaye ametaka gari hilo litunzwe na kufanyiwa marekebisho ya mara kwa mara, naye amemshukuru Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Lyambiko, kwa kufanyia kazi ombi lao.
“Kikubwa tulitunze hili gari, nakushukuru sana GM Lyabimbo kwa hili,” amesema diwani huyo kutoka chama tawala - CCM.
Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa kituo hicho cha afya, Dkt Gibarwa Nyamhanga amesema utengenezaji wa gari hilo ni habari njema kwao.
GM Lyambiko amesema sekta ya afya ni moja ya maeneo muhimu ambayo Kampuni ya Barrick inayapatia kipaumbele kwa manufaa ya jamii inayoishi jirani na migodi huo.
“Jamii inayotuzunguka ni muhimu sana kwetu. Twendelee kushirikiana kutatua changamoto zilizopo pande zote mbili ili twende pazuri zaidi,” amesema Lyambiko katika hafla ya makabidhiano hayo ambayo pia imeshuhudiwa na watendaji wa serikali ngazi ya vijiji na kata ya Matongo.
GM Lyambiko ambaye alifuatana na na Meneja Mahusiano wa Barrick North Mara, Francis Uhadi ametumia nafasi hiyo pia kutangaza kuwa wakati wowote kuanzia sasa mgodi huo utakabidhi vifaa tiba mbalimbali venye thamani ya shilingi milioni 120 kwa ajili ya kuboresha huduma za matibabu kwa wananchi katika Kituo cha Afya Nyangoto.
Mbali na sekta ya afya, maeneo ya kijamii ambayo kampuni ya Barrick inayapa kipaumbele ni uboreshaji wa huduma za elimu, maji, miundombinu (barabara) na usalama wa chakula.
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment