NEWS

Sunday 5 March 2023

Wanavijiji waishukuru Barrick North Mara kwa kukarabati barabara yao



Na Mwandishi Wetu, Nyamongo
-----------------------------------------------------

WAKAZI wa vijiji vya Nyakunguru na Nyamwaga wameushukuru Mgodi wa Dhahabu wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, kwa msaada wa kukarabati barabara ya changarawe, inayounganisha vijiji hivyo.

Wananchi hao wakiwemo waendesha bodaboda na wanawake walionesha kufurahishwa na uboreshaji wa barabara hiyo jana, ambayo ilikuwa imechimbika mashimo na hivyo kusababisha usumbufu kwa watumiaji.

“Kwa kweli tunashukuu mgodi maana sasa hakutakuwa na mashimo na mabonde ambayo yamekuwa yanaharibu hata pikipiki zetu,” alisema Samson Mseti, mmoja wa vijana wanaosafirisha abiria na migizo kwa kutumia pikipiki katika eneo hilo.

Mseti ambaye ni mkazi wa kijiji cha Nyakunguru alisema uboreshaji wa barabara hiyo ambayo pia inatumiwa na magari yanayofanya safari zake kati ya Serengeti na Tarime, utawafanya hata bodaboda kushusha nauli kwa wateja wao.

Kwa upande wake Edward Mtundi ambaye pia anafanya shughuli za bodaboda katika maeneo yaliyo jirani na mgodi huo alisema “Naona barabara sasa inakuwa safi, tunashukuru mgodi unaturekebishia barabara, tunashukuru na tupo pamoja.”

Naye Makene Mwita, mmoja wa wanawake wakazi wa kitongji cha Nyamichele kijijini Nyakunguru, alisema barabara hiyo sasa itapitika bila kwa urahisi.

“Hii barabara kubwa sasa iko nzuri, tunashukuru mgodi lakini tunaomba pia na barabara za vichochoroni zifunguliwe,” alisema Makene.

Mkazi mwingine wa kitongi hicho aliyejitambulisha kwa jina la Brandina Chacha naye aliushukuru mgodi wa North Mara kwa kukarabati barabara hiyo, lakini akaomba pia huduma nyingine za kijamii ziendelee kuboreshwa katika kijiji chao.

“Hali ya barabara sasa ni shwari, sasa tunachoomba sana na kusisitiza ni kwamba watutengenezee visima na vituo vya afya,” alisisitiza Brandina.

Jana, Sauti ya Mara ilishuhudia katapila la Kampuni ya Barrick likichonga barabara hiyo kuanzia jirani na uwanja wa ndege hadi inapokomea lami ya barabara ya Nyamwaga.

Inaelezwa kuwa uboreshaji wa barabara hiyo ni sehemu ya juhudi zinazofanywa na mgodi huo kuboresha zaidi mahusiano yake na wakazi wa vijiji 11 vilivyo jirani nao.

Vijiji hivyo kwa sasa vinashuhudia kasi ya utekelezaji wa miradi ya kijamii inayogharimiwa na mabalioni ya fedha chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Huduma za Kijamii (CSR) kutoka Kampuni ya Barrick.

Miradi inayopewa kipaumbele kupitia mpango huo wa CSR ipo kwenye maeneo matano; ambayo ni elimu, afya, usalama wa chakula, maji na uchumi.

Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Kampuni ya Barrick ilianza kutenga mabilioni ya fedha kwa ajili ya kugharimia miradi ya kijamii katika vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa North Mara mwaka 2019, ambapo kwa mara ya kwanza ilitenga dola milioni 2.5.

Aidha, kampuni hiyo ilitenga dola milioni 1.8 kwa ajili ya kugharimia miradi ya CSR kwa mwaka 2020, dola milioni 1.8 pia kwa mwaka 2021 na dola milioni 1.18 kwa mwaka 2022.

Mahusiano kati ya mgodi huo na wananchi wanaoishi katika vijiji 11 vilivyo jirani nao kwa sasa yanaripotiwa kuimarika ukilinganisha na miaka ya nyuma, kwa mujibu wa viongozi wa vijiji hivyo.

Chanzo: SAUTI YA MARA

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages