NA GHATI MSAMBA, Serengeti
------------------------------------------------
BARAZA la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti limepitisha rasmu ya mpango wa bajeti ya matengenezo mbalimbali ya barabara - ya shilingi bilioni 14.268 kwa mwaka wa fedha 2023/2024.
Madiwani hao waliridhia bajeti hiyo katika kikao cha baraza lao cha kupitisha bajeti ya TARURA kilichofanyika chini ya Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti, Ayub Mwita Makuruma kwenye ukumbi wa mikutano wa halmashauri hiyo mjini Mugumu, wiki iliyopita.
Hata hivyo Kaimu Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) Wilaya ya Serengeti, Mhandisi Charles Marwa alitaja vikwazo wanavyokutana navyo wakati wa utekelezaji wa miradi kuwa ni pamoja na uharibifu wa miundombinu ya barabara kwa baadhi ya maeneo kutokana na shughuli za binadamu, hasa kilimo, ufugaji na ukomo wa bjeti usioendna na mahitaji halisi ya kazi husika.
Mhandishi Marwa alitaja vikwzo vingine kuwa ni ukosefu wa ofisi ya TARURA Wilaya ya Serengeti, upungufu wa vitendea kazi, uharibifu wa miundombinu ya barabara kutokana na mvua na magari makubwa yenye uzito wa tani zaidi ya 10.
Alisema hatua wanazochukua ni pamoja na kujenga mitaro ya maji, kuweka vigingi vya kulinda maeneo ya hifadhi za barabara na kuelimisha wananchi juu ya kulinda miundombinu ya barabara.
Licha ya kupitisha bajeti hiyo mdiwani hao walisema baadhi ya barabara katika maeneo ya kata zao haziridhishi, na hivyo kumuomba Mhandisi Marwa kuziingiza kwenye mpango wa matengenezo ya barabara.
Diwani wa Kata ya Manchira, Joseph Kitanana alimuomba pia Mbunge wa Serengeti, Amsabi Mrimi kupeleka ushawishi Bungeni ili liwe linapitisha bajeti inayokidhi mahitaji ya matengenezo ya miundombinu ya barabara za jimbo hilo.
Chanzo: SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment