NEWS

Friday, 26 May 2023

Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa wa Mara kuzinduliwa rasmi Tarime kesho



Na Mwandishi Wetu, Tarime
----------------------------------------

LIGI ya Mpira wa Kikapu (Basketball) Mkoa wa Mara inatarajiwa kuzinduliwa rasmi wilayani Tarime kesho Jumapili.

Uzinduzi huo utafanyika katika viwanja vya Chuo cha Ualimu Tarime kuanzia saa 4:00 asubuhi, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mkuu wa Wilaya, Kanali Michael Mntenjele.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Kikapu Mkoa wa Mara, Sylvanus Gwiboha (pichani juu), mashindano ya ligi hiyo yalianza Mei 7, mwaka huu, na yanashirikisha timu saba zikiwemo nne za wanaume na tatu za wanawake.

“Wilaya ya Tarime ina timu tatu; ambazo ni Young Vita Basketball iliyoshika nafasi ya pili msimu uliopita, North Mara Basketball iliyoshika nafasi ya tatu na Tigress ya wanawake ambayo ni mpya iliyoanza kushiriki mwaka huu wa 2023,” alisema Gwiboha katika mazungumzo na Mara Online News mjini Tarime, jana.

Alisema timu za wilayani Musoma ni nne; ambazo Mwembeni Basketball ya wanaume ambayo ni bingwa msimu wa 2022, Fox Basketball iliyoshika nafasi ya nne, Tanesco Queens iliyotwaa ubingwa upande wa wanawake na Fox Divas ya wanawake ambayo ni mpya iliyoanza kushiriki msimu huu.

Gwiboha alibainisha kuwa mshindi wa kwanza wa mashindano ya ligi hiyo mwaka huu atapewa zawadi shilingi 250,000, wa pili shilingi 200,000 na watatu shilling 150,000 kwa timu zote za wanaume na wanawake.

Wakati huo huo, Mwenyekiti huyo alisema Ligi ya Mpira wa Kikapu Mkoa inatafuta wafadhili wa kuchangia uendeshaji wake.

Aliwataja wafadhili walionesha nia ya kuipiga jeki ligi hiyo mpaka sasa kuwa ni Mgodi wa Dhahabu wa North Mara, Benki ya CRDB Musoma na Tarime, NBC Tarime, Mbunge wa Tarime Mjini na wadau binafsi wakiongozwa na Martin Warioba, Miyasi pamoja na vilabu vyenyewe kuchangia ada ya ushiriki.

“Ligi hii ni moja ya ligi zenye upinzani mkubwa katika ngazi ya mkoa, tunakaribisha wadau wajitokeze kujionea viwango vya wachezaji na kutoa support (msaada) kuendeleza vipaji,” alisema Gwiboha.

Gwiboha alitumia nafasi hiyo pia kuishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kuendelea kuweka mazingira mazuri ya michezo, ikiwemo kuruhusu mashindano ya mpira wa kikapu katika shule za msingi. “Hii itafanya mchezo huu kukua,” alisema.

“Naomba serikali iangalie mkoa wa Mara katika michezo kutokana na mkoa huu kuwa na historia nzuri ya viongozi waasisi wa nchi hii, mfano, Baba wa Taifa Mwalimu JK Nyerere na wengine wengi waliotumikia nchi hii,” alisema Gwiboha.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages