NEWS

Tuesday 16 May 2023

Siku ya Familia Duniani: Shirika la Hope for Girls, Halmashauri Serengeti wakemea unyanyasji wa kijinsia, mmomonyoko wa maadili kwa watotoNa Mara Online News
---------------------------------

SHIRIKA la Hope for Girls and Women Tanzania (HGWT) limeshirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti mkoani Mara kuadhimisha Siku ya Familia Duniani, na kutumia nafasi hiyo kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia na mmomonyoko wa maadili katika jamii.

Katika hotuba yake kwenye maadhimisho hayo yaliyofanyika mjini Mugumu leo Mei 16, 2023, mgeni rasmi - Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji (pichani juu aliyesimamaa) amezihimiza familia kuzingatia suala la malezi na matunzo bora kwa watoto.

Awali, Mkurugenzi wa Shirika la HGWT, Rhobi Samwelly amesema maadhimisho hayo yana umuhimu mkubwa katika wilaya ya Serengeti yenye matukio mengi ya unyanyasji wa kijisia na mporomoko wa maadili katika baadhi ya familia.

“Sisi kama walezi, kama wazazi tumeona kwamba ni siku muhimu, tufanye maadhimisho na tuulizane tuna- fail (tunashindwa) wapi, je ni nini kinachosababisha kunakuwepo na mmomonyoko wa maadili katika familia zetu na watoto wetu, na ni mambo gani tunatakiwa kusimama nayo ili tuweze kuboresha maadili ya watoto wetu katika familia zetu,” amesema Rhobi.
Rhobi Samwelly akizungumza wakati wa maadhimisho hayo

Aidha, wadau wametumia madhimisho hayo kujadili mila na desturi zenye madhara katika jamii, lakini pia jinsi baadhi ya wazazi na walezi wanavyochangia mmomonyoko wa maadili na namna ulivyoathiri watoto katika familia na jamii kwa ujumla.

“Tumeona kuna mila na desturi nzuri, lakini kuna mila na desturi zenye madhara kwa watoto wetu - awe wa kike ama awe wa kiume. Mfano, kijana mdogo analazimishwa aozwe wanawake zaidi ya mmoja kwa sababu tu anatakiwa kurithi mila na desturi.

“Kijana mdogo anapoozeshwa wanawake zaidi ya mmoja hata kama ana ndoto yake ya kuendelea na masomo hawezi tena, atakomea kubaki pale akiwa na familia kubwa inayomwelemea, anaathirika kisaikolojia - matunzo kwa watoto yanakuwa hayapo.

“Kupitia nyumba salama tunapokea watoto wa kike ambao wamefanyiwa ukatili wa aina tofauti, lakini ukiangalia kuna uvunjifu wa maadili. Kwamba ndani ya familia hakuna maadili mazuri, yawezekana baba kambaka biti yake, baba kampa mimba binti yake, wengine kaka amembaka dada yake, na aina nyingine za mmomonyoko wa maadili,” amesema Rhobi.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages