NEWS

Wednesday 7 June 2023

Professor Mwera Foundation yawa mwenyeji wa mkutano wa vijana zaidi ya 800 kutoka ASSA mikoa ya Simiyu na Mwanza



Na Mwandishi Wetu
Mara Online News
------------------------------

TAASISI ya Professor Mwera (PMF) iliyopo Tarime mkoani Mara imekuwa mwenyeji wa mkutano wa mwaka wa vijana 870 wa Chama cha Wanafunzi wa Shule za Sekondari wa Kisabato (ASSA) kutoka mikoa ya Simiyu na Mwanza.

Mkutano huo wa siku saba ulianza Juni 4 na unatarajiwa kuhitimishwa Juni 10, mwaka huu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Tarime kinachomilikiwa na taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Vijana Jimbo la Nyanza Kusini, Isaacs Manyonyi, vijana wanaoshiriki mkutano huo ni kutoka shule za sekondari za serikali, dini na watu binafsi.

“Lengo la mkutano huu ni kuwapatia vijana hawa mafunzo ya kuwaandaa kuwa raia wema katika nchi yao na katika ufalme wa mbinguni,” amesema Manyonyi katika mazungumzo na Mara Online News chuoni hapo, leo Jumatano Juni 7, 2023.

Amefafanua kuwa mafunzo hayo yamejikita katika mada za kuwajenga vijana hao kitaaluma, kimwili, kiroho na kimaadili.
Mkurugenzi Manyonyi (katikati) katika picha ya pamoja na viongozi wenzake wanaotoa mafunzo hayo.
“Kwenye mada ya kitaaluma wanafunzi hawa wanafundishwa kuwa wasikivu na kusoma kwa bidii. Mada ya kimwili wanafundishwa mabadiliko ya kimwili, michezo na mazoezi - maana Mungu anapenda vijana wenye afya.

“Kwa upande wa kiroho wanafundishwa masuala ya Biblia na kimaadili wanafundishwa kutokubali kujihusisha na vitendo vichafu kama vile ushoga. Sambamba na hayo wanafundishwa masuala ya mahusiano na namna ya kushirikiana na watu wengine katika jamii,” amesema Manyonyi.

Kwa upande wao, vijana hao wamewashukuru viongozi wa Waadventista Wasabato waliowaandalia mkutano huo wa mafunzo, wakisema yatakuwa na faida kubwa kwao kutokana na kugusa nyanja zote za maisha.

“Pamoja na faida nyingine, mafunzo haya yatatufanya tuwe karibu na Mungu,” amesema Agnes Jackson kutoka Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa mkoani Simiyu.

Naye Tumaini Yohana kutoka Shule ya Sekondari Simiyu, amesema mafunzo hayo pia yatawawezesha kujua vipaji vyao na namna ya kuvitumia vizuri kwa manufaa ya jamii nzima.

Mkurugenzi wa Professor Mwera Foundation, Hezbon Peter Mwera amewashukuru viongozi wa Kanisa la Waadventista Wasabato kuchagua chuo chake kuwa mwenyeji wa mkutano huo wa mafunzo kwa vijana hao wa ASSA.

“Taasisi ya Professor Mwera tumefurahi kupokea na kukaribisha ugeni huu mkubwa, hii ni baraka kwetu. Pamoja na mafunzo yao, watapata pia nafasi ya kufahamu fani zinazofundishwa hapa, na tunaamini watakaporejea kwao watatusaidia kutangaza Chuo chetu cha Mafunzo ya Ufundi Tarime,” amesema Hezbon ambaye pia ni Mwenyekiti wa Wakuu wa Vyuo vya Ufundi Kanda ya Ziwa.

Fani zinazofundishwa katika chuo hicho ni pamoja na ufundi magari, uchomeleaji, udereva, ICT, kompyuta, ukatibu muhtasi, usimamizi wa hoteli na utalii, usaidizi katika maabara na uendeshaji biashara.

Hivi karibuni, Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) iliipatia Taasisi ya Professor Mwera kibali cha kufanya kazi zake na mikoa yote nchini baada ya kufanya vizuri katika mikoa 10 ya awali.

Awali, ilikuwa imepewa na Serikali kibali cha kufanya kazi katika mikoa 10; ambayo ni Mara, Mwanza, Shinyanga, Kagera, Geita, Simiyu, Kigoma, Katavi, Rukwa na Ruvu.
Mkurugenzi Hezbon Peter Mwera
“Taasisi yetu ni non-profit (isiyotafuta faida) inayojishughulisha na elimu kuanzia shule za msingi, sekondani na vyuo vya mafunzo ya ufundi. Tunahamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi, tunatambua umuhimu wa vijana kupata elimu ya mafunzo ya ufundi.

“Pia tunashirikiana na ofisi za wakuu wa mikoa kutoa tuzo na zawadi mbalimbali kwa wanafunzi wanaofanya vizuri katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha nne na cha sita,” anasema Hezbon.

Siku chache zilizopita, Taasisi ya Professor Mwera ilimtunuku Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan tuzo maalumu ya heshima kutambua mchango wake mkubwa katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Hezbon alikabidhi tuzo hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule kwa ajili ya kuifikisha kwa Rais Samia, wakati wa kikao kazi cha wadau wa elimu wa mkoa huo kilichofanyika mkoani humo.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Hezbon, PMF imejikita zaidi katika kuhamasisha vijana kujiunga na vyuo vya ufundi wakati wanasubiri matokeo ya mitihani ya kuhitimu kidato cha nne na sita, na hata darasa la saba ili kupata stadi za ufundi zitakazowawezesha kujiajiri, au kuajiriwa na hivyo kuondokana na utegemezi katika familia na jamii kwa ujumla.

Taasisi hiyo inatoa mafunzo ya ufundi kwa vijana kupitia chuo chake kijulikanacho kwa jina la Tarime Vocational Training College kilichopo mjini Tarime, chenye uwezo wa kuhudumia vijana 1,000 kwa wakati mmoja.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages