NEWS

Sunday, 23 July 2023

AICT, Right to Play wataka mtoto wa kike aondolewe vikwazo vya elimu


Afisa Miradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota (kushoto) na Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwl James Magige wikabidhi kombe kwa mwanafunzi mwakilishi wa washindi.
-----------------------------------------------------
Na Ernest Makanya, Tarime

------------------------------------

JAMII imehamasishwa kuzingatia umuhimu wa elimu iliyo bora na jumuishi kwa watoto wa kike ili waweze kuwa msaada kwa taifa siku za usoni.

Hayo yalisisitizwa na Kanisa la AICT dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Right to Play, kupitia tamasha la michezo kwa wanafunzi shule za msingi tatu katika kata ya Nyasincha wilayani Tarime, Mara juzi.


Akihamasisha jamii wakati wa tamasha hilo, Afisa Miradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Rebeca Bugota alieleza faida za elimu kwa watoto wa kike kuwa ni pamoja na kuwaandaa watu watakaolisaidia taifa kupiga hatua za maendeleo.

“Unapompa (mtoto wa kike) elimu unasaidia kuwa na taifa imara lenye maendeleo ambalo kesho na keshokutwa tutakuwa na maendeleo kwenye taifa na kijiji, kwa sababu unakuwa umepandikiza kwao elimu inayoweza kuwasaidia,” alisema Rebeca.


Rebeca akizungumza wakati wa tamasha hilo

Aidha, Rebeca alitaja ndoa za utotoni, ukeketaji na majukumu mengi ya nyumbani kuwa ni miongoni mwa vikwazo vya elimu kwa wasichana, na hivyo akatumia nafasi hiyo pia kutoa wito kwa jamii nzima kusaidia kubadili utamaduni huo.

“Tuwatie moyo kwa sababu wakati mwingine jamii inamtazama mtoto wa kike kwamba ataishia kuolewa tu, lakini hata kama akiolewa akiwa na elimu atatengeneza familia iliyo imara. Kwa hiyo tuwasaidie kubadilisha ule mtazamo ili nao wajione wanaweza kusoma na kufika mbali na wakalifaa taifa hili,” lisisitiza Rebeca.

Naye Afisa Elimu Kata ya Nyansincha, Mwl James Magige aliunga mkono hoja hiyo akisema “Ili mtoto wa kike aweze kupata haki yake ni lazima aweze kupata elimu, atakapoingizwa kwenye ushindani aonekane anafaa katika idara au kazi anayotakiwa kuchukua.”

Kwa mujibu wa Rebeca, Shirika la Right to Play linatekeleza mradi wa maboresho ya elimu kupitia michezo, midahalo na kuwajengea uwezo walimu na wanafunzi katika kata za Nyasincha, Itiryo na Nyamwaga zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages