NEWS

Sunday 23 July 2023

Mkulima adai kuporwa ardhi, kuharibiwa mazao kijijini Kemakorere



Na Joseph Maunya, Tarime
-----------------------------------

MKULIMA na mkazi wa kijiji cha Kemakorere wilayani Tarime, Mwita Chacha Paulo amedai kuporwa kimabavu ardhi yenye ukubwa wa ekari 40, na kuharibiwa mazao mbalimbali ya chakula.

“Wamenifyekea ekari nne za mahindi, magimbi ekari mbili, mihogo ekari mbili na kuna watu waliokodi mashamba kwenye langu nao wamefyekewa viazi ekari mbili, na sasa hivi wavamizi wameweka ng'ombe wanachunga.

“Sasa hivi sina hata kitu cha kuwapa watoto, wamefyeka mazao yote ya vyakula niliyokuwa limelima. Ninaomba Serikali itusaidie inirudishie vyote vilivyoharibiwa ili nipate cha kuwapa hata watoto,” alilalamika Paulo wakati akizungumza na waandishi wa habari kijijini hapo, wiki iliyopita.


Kuhusu ardhi anayodai kuporwa, ambaye ni mlemavu wa viungo alisema alirithishwa ardhi hiyo na baba yake, na kwamba kabla ya hapo ilikuwa mali ya babu yake tangu mwaka 1942.

Kwa mujibu wa Paulo, mwaka 2018 alishinda kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza na kukabidhiwa ardhi hiyo kihalali.

"Nilishinda kesi katika Mahakama Kuu Kanda ya Ziwa, baadaye nikaenda kwa Mkuu wa Mkoa (wa Mara wakati huo) Ali Hapi akaelekeza nirejeshewe eneo langu kama mahakama ilivyoagiza,” alisema.

Katika hatua nyingine, Paulo amedai kusiai kusikitishwa na kitendo cha dalali aliyemtaja kwa jina la James Mahando aliyepewa jukumu la kuondoa wavamizi katika ardhi yake tangu mwaka 2019, ambapo sasa anamtuhumu kuwa amewarudisha tena Julai mwaka huu na kufyeka mazao ya chakula aliyokuwa amelima.

Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kemakorere, Chacha Manga alipouliwa alikiri kuwepo kwa mgogoro wa muda mrefu katika eneo hilo, na kwamba hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliamuru Mwita Chacha Paulo kupimiwa eneo lake la heka 40, ambapo vipimo vilionesha eneo hilo lina ukubwa wa ekari 75.

Hata hivyo, Manga alisema ofisi ya Serikali Kijiji hicho haijapata nyaraka za kisheria za kumilikishwa ekari 35 zilizozidi kama inavyodaiwa na baadhi ya watu.

Kwa upande wake, dalali Mahando amezungumza na Mara Online News na kukana tuhuma za kupeleka wavamizi katika eneo la Paulo.
 
Badala yake Mahando amesema alichokifanya ni utekelezaji wa maamuzi ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza, kwa kumkabidhi Paulo ardhi aliyokuwa akidai - yenye ukubwa wa ekari 40 kijijini Kemakorere.
 
"Tulienda na Mpima kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, tukampimia ekari 40 alizokuwa anadai na tumeshaandikisha taarifa za utekelezaji wa maamuzi hayo ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza," amesema Mahando.
 
Kuhusu mazao yanayodaiwa kuharibiwa, Mahando amesema ni ambayo Paulo aliyapanda kwenye eneo ambalo bado lilikuwa na mgogoro.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages