NEWS

Thursday 24 August 2023

Kilichovunja mkutano wa bodaboda Tarime Mjini, wabunge Esther Matiko, Kembaki watajwa
Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News, Tarime
------------------------------------


KATIKA tukio lisilo la kawaida, mkutano wa waendesha pikipiki “bodaboda” uliokuwa ufanyike mjini Tarime siku chache zilizopita, ulivunjika kabla ya kufikia malengo yake, imebainika. 

Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Michael Kembaki (CCM) na Mbunge wa Viti Maalum, Esther Matiko (CHADEMA) wanatajwa kuwa chanzo cha kuvunjika kwa mkutano huo, baada ya kubainika kwamba walialikwa kuuhudhuria. 

Inaelezwa kuwa kitendo cha kuwagonganisha mahasimu hao wa kisiasa kingeweza kuukosesha mkutano huo ‘afya’ ya kufikia malengo yake. 

“Lengo la mkutano wetu lilikuwa zuri, ilikuwa ni kujenga umoja wa bodaboda kupitia wabunge wetu lakini sasa siasa ikaingilia,” Katibu wa Umoja wa Bodaboda Wilaya ya Tarime, Dickson Rhobi ameiambia Mara Online News leo. 

Dickson amesema wabunge wote hao kila mmoja alipata mwaliko wa kushiriki katika mkutano huo ambao ulipangwa kufanyika kwenye ukumbi wa CMG Hotel mwanzoni mwa Agosti 2023. 

“Tulitaka pia tuwaeleze changamoto zetu kama bodaboda lakini ndio hivyo, ilivyoleta sintofahamu tukahairisha mkutano, tutapanga upya,” amesema kiongozi huyo. 

Ameongeza kuwa umoja wa bodaboda ulitegemea upate mchango kutoka kwa wabunge hao lakini haikuwezekana. 

“Hata ukumbini hakuna mbunge aliyefika, kwetu ilikuwa pigo maana hatuna hata ofisi. Tutajipanga upya kuwaita kila mtu kwa wakati wake maana hawawezi kukaa pamoja,” amesema. 

Mara Online News inaendelea na juhudi za kuwapata wabunge hao kwa ajili ya kupata kauli zao juu ya suala hilo. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages