NEWS

Monday 28 August 2023

Mashindano ya Tiboche Cup yaingia dosari, jezi zadaiwa kuchanwa, Mwenyekiti CCM Wilaya ya Tarime aeleza kilichotokea




Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News
---------------------------


KATIKA tikio lisilo la kawaida, mashindano ya soka ya ‘Tiboche Cup’ yameingia dosari, ambapo baadhi ya jezi za wachezaji zimedaiwa kuchanwa, huku benchi la ufundi likidaiwa kuingiliwa na siasa. 

Fainali ya mashindano hayo yaliyoandaliwa na Diwani wa Kata ya Nyanungu, Tiboche Richard, ilikuwa ichezwe jana Jumapili kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Mangucha, lakini ikashindikana. 



Inaelezwa kuwa chanzo cha kuchanwa kwa baadhi ya jezi za wachezaji ni mvutano ulioibuka kati ya timu ya Nyamombara na ya Mangucha ambazo zilituhumiana kuchezesha wachezaji ambao hawakukidhi vigezo vya mashindano hayo. 

“Wachezaji na mashabiki waliona badala ya hasira za kushambulia mtu bora wachane jezi kwa kutumia visu,” ameeleza mmoja wa mashabiki waliojitokeza uwanjani kwa ajili ya kutazama na kushangilia mashindano hayo. 

Alipoulizwa na Mara Online News kwa njia ya simu leo Jumatatu, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho aliyekuwa mgeni rasmi katika mashindano hayo, amesema aliwasili uwanjani akakuta timu hizo zinavutana na kwamba yeye hakuwa chanzo cha kuchanwa kwa jezi za wachezaji. 

“Ni kweli jezi zilichanwa lakini chanzo sio mimi mgeni rasmi. Nilifika nikakuta mgogoro unaendelea, kuuliza nikambiwa kuna mchezaji wa timu moja hakusajiliwa na wa timu nyingine siyo mkazi wa kijiji. Kwa hiyo mgogoro ulikuwa wa timu, siyo mimi,” Ngicho amefafanua. 



Aidha, baadhi ya wachezaji na mashabiki wa mashindano hayo ya ‘Tiboche Cup’ wamelaumu kile walichokiita benchi la ufundi kutawaliwa na siasa. 

Hivyo mechi ya fainali ya mashindano hayo - kati ya timu ya Mangucha na Nyamombara iliahirishwa kutokana na tafrani hizo, hadi itakapopangiwa tarehe nyingine. 

Viongozi wengine waliokuwa wamehudhuria mashindano hayo ni pamoja na Katibu wa Mbunge wa Tarime Vijijini, Remmy Mkapa aliyemwakilisha Mbunge Mwita Waitara katika mashindano hayo. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages