NEWS

Tuesday 8 August 2023

Tume ya Madini yainoa migodi ya Barrick ushirikishwaji wa Watanzania sekta ya madiniNa Mwandishi Maalumu, Nyamongo
-------------------------------------------------

TIMU ya wataalamu kutoka Tume ya Madini leo inaendesha warsha ya mafunzo kwa migodi ya Barrick kuhusu ushirikishwaji wa Watanzania kwenye sekta ya madini ili waweze kupata fursa zaidi za kutoa huduma katika migodi ya kampuni hiyo nchini. 

Warsha hiyo inayofahamika kama 'Local Content Workshop' inaendelea leo katika Mgodi wa Dhahabu Barrick North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, Mara ambapo pia mada ya utekelezaji wa miradi ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) itapewa kipaumbele.Washiriki wa warsha hiyo ni kutoka migodi ya North Mara na Bulyanhulu uliopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, lakini pia kutoka ofisi ya Barrick jijini Dar es Salaam. 

Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema ujio wa warsha hiyo ni muhimu katika kuimarisha na kuboresha ushirikishwaji wa Watanzania katika kutoa huduma mabalimbali mgodini hapo. 
“Mategemeo yetu ni kwamba tutakuwa na maboresho baada ya ujio wenu,” GM Lyambiko alisema katika sehemu ya hotuba yake fupi jana. 

Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Madini na Biashara kutoka Tume ya Madini, Andrew Mgaya alipongeza mgodi wa Barrick North Mara kwa kuendelea kuwekeza kwenye miradi ya kijamii - lakini akasisitiza umuhimu wa kuhakikisha kila mradi unakuwa endelevu.
“Niwapongeze Barrick kwa juhudi hizi lakini suala la sustainability (uendelevu) kwa kila mradi ni muhimu,” alisema Mgaya ambaye ndiye kiongozi wa msafara wa maafisa hao wa Serikali kutoka Tume ya Madini.

Timu hiyo iliwasili Nyamongo jana na kupata fursa ya kutembelea na kujionea shughuli za uchimbaji madini kwenye shimo la chini (underground) katika eneo la Gokona.


Pia ilitembelea na kujionea baadhi ya miradi ya kijamii inayofadhiliwa na mgodi wa Barrick North Mara ukiwemo mradi mkubwa wa maji uliopo kijiji cha Nyangoto uliogharimu shilingi takriban bilioni moja kupitia mpango wa CSR wa Barrick North Mara, ujenzi wa shule mpya ya msingi Kenyangi katika kijiji cha Matongo na mradi wa kilimo biashara wa vijana kijijini Matongo pia.

Wakiwa katika picha ya pamoja

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages