NEWS

Tuesday 29 August 2023

UCHAMBUZI: Hakika Prof Muhongo anastahili tuzo hiiMbunge wa Jimbo la Musoma Vijiji, Prof Sospeter Muhongo.

Na Mwandishi Wetu
---------------------------


HIVI karibuni, uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Musoma mkoani Mara ulimtunuku Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof Sospeter Muhongo tuzo maalum ya heshima, ikiwa ni kutambua juhudi kubwa anazofanya za kuwaletea wananchi wa jimbo hilo maendeleo ya kisekta. 

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi alimkabidhi Prof Muhongo tuzo hiyo katika hafla maalum iliyoandaliwa na uongozi wa CCM Wilaya ya Musoma, hivi karibuni. 

Uongozi wa CCM umekuwa wa kwanza ndani ya chama hicho tawala kutambua mchango wa Prof Muhongo katika jitihada za kuwaletea wakazi wa jimbo la Musoma Vijijini maendeleo, na hivyo kumtunuku tuzo hiyo. 

Hakika Prof Muhongo anastahili tuzo hiyo kutokana juhudi zake kubwa za hali na mali anazofanya kwa maslahi mapana ya wananchi wa jimbo hilo, mkoa wa Mara na Taifa kwa ujumla. 

Tangu achaguliwe kuwa Mbunge wa Musoma Vijijini kwa tiketi ya chama tawala - CCM, Prof Muhongo amekuwa chachu ya maendeleo ya wananchi. Amedhihirisha uwezo mkubwa alio nao katika kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi ndani ya jimbo hilo. 

Leo hii huwezi kuzungumzia maendeleo ya kisekta, ikiwemo elimu, maji, barabara na kilimo katika jimbo la Musoma Vijijini bila kutaja jina la Prof Sospeter Muhongo. Ni mbunge mwenye bidii na mpenda maendeleo wa kweli kuwahi kushuhudiwa Tanzania. 

Wengi tunashuhudia na kusikia miradi ya elimu na maji ikiendelea kutekelezwa kwa kasi kubwa katika jimbo la Musoma Vijijini kutokana na jitihada za hali na mali zinazofanywa na Mbunge Muhongo. 

Ni katika kipindi cha uongozi wa Prof Muhongo ambacho tunashuhudia shule za msingi na sekondari, zikiwemo za sayansi zikiendelea kuota kama uyoga. Amekuwa mstari wa mbele katika kuchangia ujenzi na maboresho ya miundombinu ya elimu, sambamba na chakula cha wanafunzi shuleni. 

Juhudi za mbunge huyu zinaonekana pia katika kuhakikisha kuwa miradi ya huduma ya maji inasogezwa karibu na wananchi ndani ya jimbo la Musoma Vijijini. 

Lakini pia utekelezaji wa miradi ya barabara unaendelea kushika kasi, na hivi karibuni tulishuhudia ujenzi wa barabara ya kwanza kwa kiwango cha lami ukiripotiwa kukamilika katika jimbo hilo, kutokana na msukumo uliowekwa na mbunge huyu. 

Jitihada za maendeleo zinazofanywa na Prof Muhongo zimeendelea kuonekana pia katika sekta ya kilimo, ambapo mara kwa mara amekuwa akihamasisha wakulima kwa kuwapatia misaada ya pembejeo zikiwemo mbegu, mbolea na majembe ya kukokotwa na ng’ombe (plau). 

Kwa upande mwingine, Mbunge Muhongo amekuwa akijitolea kwa hali na mali kuwasaidia wavuvi kuboresha shughuli za uvuvi na kukuza kipato chao. Kwa kifupi kiongozi huyu anaifungua na kuistawisha Musoma Vijijini kila upande. 

Uongozi wa CCM Wilaya ya Musoma unastahili pongezi kwa kuona umuhimu wa kumtunuku Mbunge Muhongo tuzo ya heshima kutokana na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya wananchi Musoma Vijijini. 

Mkoa wa Mara na Tanzania kwa ujumla tunahitaji viongozi jasiri, wachapa kazi, wenye utashi na dhamira ya kweli ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kama Prof Muhongo. Hakika mbunge huyu anastahili Tuzo ya Heshima. Ni kiongozi wa aina yake. 

Na itoshe kusema kwamba mpaka sasa Prof Muhongo ndiye mbunge anayeoongoza mkoani Mara kwa kusimamia na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya CCM na falsafa ya serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan - ya kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli kupitia jimbo la Musoma Vijijini. Nani anapinga? 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages