NEWS

Monday 18 September 2023

Hifadhi ya Serengeti ilivyojitangaza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Mto Mara 2023Wageni wakipata huduma kwenye banda la Maliasili na Utalii wakati wa Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara kwenye viwanja vya Sokoinne wilayani Serengeti, Tanzania.
----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------
 


HUENDA idadi ya watalii wa ndani na kigeni ikaongezeka zaidi katika Hifadhi ya Taifa Serengeti baada ya hifadhi hiyo kujitangaza vizuri katika Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara yaliyoandaliwa na nchi za Tanzania na Kenya. 

Maadhimisho hayo yalifanyika Septemba 12 hadi 15, mwaka huu kwenye viwanja vya Sokoinne vilivyopo katika mji wa Mugumu, wilaya ya Serengeti mkoani Mara, Tanzania. 

Kwa mujibu wa Mhifadhi Abed Mwesigwa kutoka Idara ya Mahusiano ya Jamii Hifadhi ya Taifa Serengeti, maadhimisho hayo yamekuwa ya manufaa kwa hifadhi hiyo kwani imeyatumia kujitangaza zaidi kwa wakazi wa mkoa wa Mara na raia wa Kenya. 

“Tumekuwa hapa kwenye banda la Maliasili na Utalii tangu Septemba 12 hadi leo tarehe 15, maadhimisho yamefanyika vizuri, wananchi wameonesha mwitikio mkubwa katika banda letu,” Mwesigwa aliliambia Gazeti la Sauti ya Mara wakati wa kilele cha maadhimisho hayo. 

Alisema wameshirikiana na wadau mbalimbali wa uhifadhi wakiwemo TAWA na Shirika la Frankfurt Zoological Society (FZS) kuonesha vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo katika Hifadhi ya Taifa Serengeti, pamoja na jitihada wanazofanya kulinda uendelevu wa ikolojia ya Serengeti inayohusisha Mto Mara. 

“Wageni wengi kutoka maeneo mbalimbali ya mkoa wa Mara na nchi jirani ya Kenya wametembelea banda letu la Maliasili na Utalii, wakiuliza maswali mbalimbali kuhusu Hifadhi ya Taifa Serengeti, hasa wakitaka kujua namna ya kufika hifadhini na gharama za utalii. 

“Wananchi wengi walikuwa wanadhani gharama za utalii ni kubwa sana, lakini tumewahakikishia kwamba gharama za kutalii katika Hifadhi ya Serengeti ni ndogo maana kiingilio ni shilingi 10,000 kwa mtu,” alisema Mwesigwa. 

Mhifadhi Mwesigwa anaamini kuwa elimu waliyowapa watu waliotembelea banda la Maliasili na Utalii wakati wa maadhimisho hayo ya Siku ya Mto Mara itasaidia kuongeza idadi ya watalii wa ndani katika hifadhi hiyo. “Mpaka sasa watalii wa kigeni ndio wengi kuliko watalii wa ndani wanaotembelea hifadhi yetu ya Serengeti,” alisema. 

Katika kuhamasisha uhifadhi na ulinzi shirikishi wa maliasili za Hifadhi ya Taifa Serengeti, Mhifadhi Mwesigwa alisema wanaendelea kutekeleza mpango wa kujenga uhusiano na ujirani mwema na vijiji vinavyozunguka hifadhi hiyo. 

Kwamba Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kupitia Hifadhi ya Taifa Serengeti linaendelea kutekeleza mpango wake wa ujirani mwema kwa kusaidia kujenga na kuboresha huduma za kijamii katika vijiji hivyo. 

Alitaja huduma hizo kuwa ni pamoja na afya, elimu na malambo ya maji kwa ajili ya matumizi ya mifugo, sambamba na kuendelea kuelimisha jamii umuhimu wa uhifadhi na ulinzi wa wanyamapori na mazingira, ukiwemo Mto Mara. 

Alisema huwezi kuzungumzia uhifadhi na umaarufu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti bila kutaja Mto Mara, na hii ni kutokana na mto huo kuwa tegemeo muhimu la maji na makazi kwa wanyamapori, wakiwemo nyumbu na mamba katika hifadhi hiyo. 

Inaelezwa kuwa wanyama wanapenda kunywa maji ya Mto Mara kwa sababu hayana magadi, na ikumbukwe pia kwamba wanyama kama vile viboko, mamba na viumbe hai wengine wanaochangia mvuto wa Hifadhi ya Taifa Serengeti wanaishi katika Mto Mara. 

Pia Mto Mara umechangia kuiingiza Hifadhi ya Taifa Serengeti kwenye orodha ya Maajabu Saba ya Urithi wa Dunia kutokana tukio la uhamaji wa nyumbu ambao huvuka mto huo kila mwaka. 

Hivyo kwa upande mwingine, Mto Mara ni miongoni mwa vivutio vya kitalii vinavyoibeba hifadhi hiyo na umekuwa chachu ya fursa za uwekezaji katika sekta za utalii na uchumi. 

Ardhi oevu ya Mto Mara yenye ukubwa wa kilomita za mraba 387 inayopatikana mkoani Mara, Tanzania inatajwa kuwa ni eneo lenye baioanuai muhimu kidunia na hutoa huduma mbalimbali za kiikolojia, ikiwemo uvuvi. 

Ndiyo maana Mhifadhi Mwesigwa anawaalika watu kutoka ndani na nje ya Tanzania kutembelea Hifadhi ya Taifa Serengeti ili kuona Mto Mara ulivyo kivutio na jinsi makundi ya wanyamapori aina ya nyumbu wanavyouvuka kwenda Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara nchini Kenya na kurudi Serengeti. 

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya 12 ya Siku ya Mto Mara mwaka huu wa 2023 inasema “Hifadhi Mto Mara kwa ustawi wa viumbe hai na uchumi endelevu”. 

Mto Mara unaanzia katika chemchem ya Enapuyapui iliyo kwenye misitu ya Milima ya Mau ambapo maji ya mto huo hutiririka kupitia Hifadhi ya Taifa ya Maasai-Mara, Kenya na Hifadhi ya Taifa ya Serengeti kabla ya kumwaga maji yake katika Ziwa Victoria upande wa Tanzania. 

Tanzania na Kenya zimekuwa zikiadhimisha kilele cha Siku ya Mto Mara Septemba 15 kila mwaka kwa kupokezana, ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za pamoja za uhifadhi endelevu wa Bonde la Mto Mara unaotiririsha maji kwenye Ziwa Victoria. 

Siku ya Mto Mara ni zao la kikao cha 10 cha Sekretarieti ya Mawaziri wa Bonde la Ziwa Victoria kilichofanyika Kigali nchini Rwanda Mei 4, 2012 ambacho kiliazimia Siku hiyo iwe inaadhimishwa Septemba 15 kila mwaka. 

Maadhimisho ya kwanza ya Siku ya Mto Mara yalifanyika mwaka 2012 nchini Kenya na kwa upande wa Tanzania maadhimisho ya kwanza ya siku hiyo yalifanyika mwaka 2013. 

Mbali na umuhimu wa uhifadhi wa wanyamapori, inakadiriwa kuwa maisha ya watu zaidi ya milioni moja hutegemea uwepo wa Bonde la Mto Mara upande wa Tanzania na Kenya. 

Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages