NEWS

Tuesday 5 September 2023

RC Mtanda atuma salamu kwa 'wapigaji' wa fedha za umma Mara, ampa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Rorya maagizo mazito

RC Said Mohamed Mtanda

Na Mwandishi Wetu –
Mara Online News
-------------------------- 


SIKU moja baada ya Gazeti la Sauti ya Mara kuripoti habari kuhusu viashiria vya ‘upigaji’ wa fedha za Serikali katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ametoa taarifa kwa umma, akisema hatafumbia macho ubadhirifu na matumizi mabaya ya fedha za umma mkoani humo. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo aliyoitoa leo Jumanne, RC Mtanda amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya kutoa ufafanuzi kwa umma kuhusiana na mambo yaliyoibuliwa na gazeti hilo. 

“Mkuu wa Mkoa wa anawahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Mkoa wa Mara inafuatilia kwa karibu mchakato mzima wa ukaguzi wa ndani uliofanyika na wale watakaobainika kuvunja sheria na taratibu za manunuzi watachukuliwa hatua za kisheria,” imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyosainiwa na Afisa Habari Mkuu, Rainfrida Ngatunga wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara. 

Jana Jumatatu, Gazeti la Sauti ya Mara ambalo ni chombo dada cha Mara Online News, lilichapisha habari kubwa inayoelezea hatua ya Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Rorya ya kumsimamisha kazi Kaimu Afisa Manunuzi wa halmashauri hiyo, Dominiani Mpombe ili kupisha uchunguzi kutokana na ukiukwaji wa taratibu kwenye ununuzi wa vifaa tiba vya maabara, vikiwemo vya tiba ya kinywa na meno vyenye thamani ya shilingi milioni 335.6. 

Baraza hilo likiongozwa na Mwenyekiti wa Halmashauri, Gerald Ng’ong’a, lilifikia hatua hiyo katika kikao chake cha kupata taarifa ya robo ya nne, yaani Aprili - Juni 2023 kilichofanyika wilayani humo Alhamisi iliyopita, baada ya kusomewa taarifa ya Mkaguzi wa Ndani inayoonesha kuwa fedha hizo zililipwa kabla ya vifaa hivyo kupokewa. 

Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya ukaguzi, kitendo cha kulipa fedha kabla ya mapokezi ya vifaa hivyo kinakiuka Mwongozo wa Fedha za Serikali wa Mwaka 2009 unaokataza kufanya malipo kabla ya huduma husika kutolewa. 

Inadaiwa kuwa baadhi ya vifaa hivyo havijapokewa kwa takriban miezi mitatu sasa baada ya malipo hayo kufanyika. 

Aidha, taarifa ya ukaguzi inaonesha kuwa Halmashauri licha ya kukata kodi ya zuio kiasi cha shilingi milioni 7.987, imeshindwa kufanya malipo hayo kwenda kwenye akauti ya Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), pamoja na ushuru wa huduma wa halmashauri. 

Katika hatua nyingine, taarifa hiyo ya ukaguzi pia imebaini ukiukwaji wa taratibu katika ununuzi wa madirisha ya aluminiamu kwa ajili ya Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, vyenye thamani ya shilingi takriban milioni 30. 

Ukiukwaji mwingine wa taratibu umebainika pia kwenye utekelezaji wa miradi ya BOOST yenye thamani ya shilingi bilioni 1.86 zilizotolewa na Serikali Kuu kwa ajili ya ujenzi wa shule mpya za msingi Mkengwa na Kinesi B zilizopo kata ya Nyamunga katika halmashauri hiyo. 

Taarifa ya ukaguzi inaonesha kuwa baadhi ya manunuzi ya vifaa vya ujenzi hayakufuata taratibu, hali ambayo pia imesababisha ununuzi wa vifaa vingi zaidi ya mahitaji. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages