NEWS

Friday 1 September 2023

Right to Play, AICT wapigania elimu ya mtoto wa kike Tarime, SerengetiDiwani wa Kata ya Rigicha wilayani Serengeti, Moranya Baruti akikabidhi kombe kwa kapteni wa timu ya wasichana ya mpira wa pete ya Shule ya Msingi Wagete wakati wa tamasha la michezo lililoandaliwa na Shirika la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe katani humo, hivi karibuni. Kushoto ni Afisa Mradi kutoka AICT, Rebeca Bugota.
----------------------------------------------------

Na Waandishi Wetu,
Tarime na Serengeti
---------------------------


SHIRIKA la Right to Play limeendelea kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kupaza sauti ya umuhimu wa elimu kwa watoto wa kike. 

Kupitia tamasha la michezo mbalimbali kwa wanafunzi wa shule za msingi Kimusi na Nyamiri zilizopo Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, wanafunzi, wazazi na walezi wamehamasishwa kusaidia watoto wa kike kupata elimu. 

“Tuwape watoto wa kike nafasi ya kusoma sawa na watoto wa kiume. Watoto wa kike wamekuwa wakikutana na vikwazo kama vile ukeketaji, ndoa na mimba za utotoni, hivyo sote kwa pamoja tushikamane kumtetea mtoto wa kike apate elimu,” Mratibu wa Mradi kutoka Right to Play, Onesmo Singo alisema wakati wa tamasha hilo lililofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Kimusi hivi karibuni. 


Mratibu wa Mradi kutoka Right to Play, Onesmo Singo akizungumza wakati wa tamasha hilo

Kwa upande wake Kaimu Mratibu Elimu Kata ya Nyamwaga, Mwl Jacob Peter alisema “Tunasisitiza elimu kwa watoto wa kike siyo kwa sababu wao ni wa pekee, hapana, ila ni kwa sababu wao wanakumbwa na changamoto nyingi.” 

Naye Afisa Mtendaji Kijiji cha Kimusi, John Marwa Matete aliyekuwa mgeni rasmi katika tamasha hilo, alisema elimu itawezesha watoto wa kike kupata nafasi ya kufanya kazi katika ofisi za umma, kwa idadi kubwa kama ilivyo kwa wanaume. 

“Nimejifunza umuhimu wa sisi watoto wa kike kupata elimu, lakini pia leo tumecheza michezo mbalimbali yenye faida kubwa kwa afya zetu,” alisema Veronika Koroso Musiani, mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Nyamiri. 

Kutoka wilaya ya Serengeti, Mwandishi Wetu anaripoti kuwa Shirika hilo la Right to Play kwa kushirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe wanatekeleza mradi wa ‘Save Her Seat’ kuhamasisha wazazi na walezi wilayani Serengeti kusomesha watoto wa kike, ili waweze kutimiza ndoto zao za kielimu na maisha katika jamii. 

Akitoa elimu hiyo kupitia tamasha la michezo kwa wanafunzi lililofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Wagete wilayani Serengeti hivi karibuni, Afisa Mradi Mradi kutoka AICT, Rebeca Bugota alisema uwekezaji kwenye elimu ya mtoto wa kike unalipa. 

“Kuwasaidia watoto wa kike wafike kwenye mafanikio yao ni jukumu la mzazi, huwezi kuvuna mahala usipopanda - wala mazao mazuri kwenye shamba ambalo huwezi kulihudumia. Kama tunataka matokeo mazuri lazima tuwekeze kwenye elimu ya watoto wa kike sawa na wa kiume,” alisema Rebeca. 

Mwenyekiti wa Kamati ya Shule ya Msingi Wagete, Gideon John alikazia hoja hiyo akiwataka wakazi wa kijiji hicho kubadilika kwa kusomesha watoto wa kike ili waweze kuwa hazina ya baadaye. 

“Ukisomesha mtoto wa kike ni tofauti na aliyesomesha mtoto wa kiume, mtoto wa kike anaweza kuleta manufaa makubwa, hivyo tubadilike na kuelewe kuwa unapomsomesha mtoto wa kike ni hazina,” alisema Gideon. 

Diwani wa Kata ya Rigicha, Moranya Baruti alilishukuru na kulipongeza Shirika la Right to Play na AICT kwa kuona umuhimu wa kupeleka hamasa ya elimu kwa mtoto wa kike wilayani Serengeti. 

Naye Mchungaji Joseph Daudi wa Kanisa la Tanzania Assembles of God (TAG) la kijijini Wagete, alisema hakuna jamii inayoweza kuendelea na kuwa bora kwa kumwacha nyuma mtoto wa kike. 

“Ukimwona mwanaume mwenye mafanikio kuna mwanamke mwenye nguvu nyuma yake, hivyo watoto wa kike na wa kiume wapewe fursa sawa ya kupata elimu ili tuweze kuwa na jamii iliyo bora,” alisema Mchungaji Joseph. 

Kaulimbiu ya tamasha hilo la michezo inasema "Elimu kwa Wasichana kwa Kesho Endelevu, Tuwalinde na Kuwapa Fursa Sawa." 

Shirika la Right to Play linashirikiana na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe katika kuendesha/ kusimamia mradi wa Tunza Nafasi ya Msichana, kupitia matamasha ya michezo katika baadhi ya shule za msingi zilizopo Halmashauri za Wilaya za Tarime na Serengeti mkoani Mara. 

Aidha, lengo kuu la tamasha la michezo kwa wanafunzI chini ya mradi wa ‘Save Her Seat’ unaotekelezwa katika wilaya ya Serengeti, ni kuikumbusha jamii kuacha mfumo dume, mila na desturi potofu, na hivyo kumlinda na kumwezesha mtoto wa kike kupata elimu na fursa sawa na mtoto wa kiume.

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages