NEWS

Wednesday 6 September 2023

Uzinduzi Kiles Cup: Magoto FC yaichapa Kebweye FC 2-1 Tarime Vijijini



Mkwaju wa penati ulioipa ushindi Magoto FC dhidi ya Kebweye FC.

Na Godfrey Marwa –
Mara Online News
---------------------------


TIMU ya Magoto FC imeibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Kebweye FC katika mechi ya uzinduzi wa mashindano ya soka ya Kiles Cup, iliyochezwa katika uwanja wa Shule ya Sekondari Magoto wilayani Tarime, Mara jana Jumanne. 

Mashindano hayo yanadhaminiwa na Diwani wa Kata ya Nyakonga, Simion Kiles ambaye pia ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 


Katibu wa CCM Wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji akikagua timu uwanjani.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mashindano hayo, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime, Noverty Kibaji aliyekuwa mgeni rasmi, alimpongeza Kiles kwa kutekeleza agizo la chama hicho tawala.

“Tuliagiza sisi kamati ya Siasa ya Wilaya kwamba waheshimiwa madiwani wasimamie na kutekeleza Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa kufufua michezo katika kata zote. Mwaka 2024 na 2025 kupitia michezo tuna hakika tutawapata vijana watakaopiga kura kwa CCM wenye afya njema,” alisema Kibaji. 

Ukaguzi wa timu ukiendelea

Naye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Marema Sollo aliwataka vijana wanaoshiriki mashindano hayo kutumia fursa hiyo kujijenga kisoka na hatimaye ikiwezekana waweze kuchezea timu kubwa. 

“Michezo ni furaha, ni burudani, tunataka kuwaona wenye vipaji na tutengeneze timu ya kata. hatutegemei mkomee hapa, tunataka mwende mbali, ukicheza vizuri pengine tukashangaa kuona uko timu zinazocheza Ligi Kuu kama Azam au Ihefu,” alisema Marema. 

#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages