NEWS

Monday 30 October 2023

Twiga yang’ara Usiku wa Madini, yashinda Tuzo ya Juu ya Kuchangia Pato la SerikaliWaziri wa Madini wa Malawi, Monica Chang'anamuno (kushoto) akikabidhi Tuzo ya Juu ya Kuchangia Pato la Serikali kwa Afisa Mawasiliano wa Twiga Minerals Corporation, Abella Mutiganzi (katikati) kwa niaba ya kampuni wakati wa hafla ya Usiku wa Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni. Kulia ni Waziri wa Madini, Antony Mavunde.
-------------------------------------

Na Mwandishi Wetu
---------------------------
 

UBIA wa Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga na Kampuni ya Dhahabu ya Barrick, unazidi kuleta mafanikio mbalimbali, ambapo katika hafla ya Usiku wa Madini iliyofanyika hivi karibuni, Twiga imefanikiwa kushinda Tuzo ya Juu ya Kuchangia Pato la Serikali, pamoja na Tuzo Maalum ya Umiliki wa Leseni ya Uchimbaji wa Madini (Special Mining License Holder Awards). 

Tuzo hizo zilitolewa na Wizara ya Madini ambayo iliandaa hafla hiyo, na zilikabidhiwa na Waziri wa Madini wa Malawi, Monica Chang'anamuno, kwa kushirikiana na Waziri wa Madini Tanzania, Antony Mavunde ambaye aliipongeza Twiga kwa kuendelea kufanikisha kuleta mapinduzi makubwa ya maendeleo nchini kupitia uwekezaji katika sekta ya madini, kupitia migodi yake ya Bulyanhulu na North Mara. Tangu mwaka 2019 ilipoichukua migodi hiyo iliyokuwa imekufa, Barrick imeibadilisha na kuifanya kuwa na viwango vya kimataifa, na vilevile kampuni imechangia zaidi ya dola bilioni tatu katika uchumi wa Tanzania, ambapo mwaka huu Twiga ilitambuliwa kuwa mlipaji mkubwa wa gawio kuliko kampuni zote ambazo Serikali ina maslahi nazo. 

Migodi ya Barrick pia hutumia asilimia 84 ya bajeti yake ya manunuzi kwa kampuni za ndani, huku asilimia 96 ya nguvu kazi yake ikiwa ni ya wananchi wa Tanzania. 

Kupitia sera ya Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), kampuni imeishatumia kiasi cha Dola za Kimarekani milioni 13.2 kutekeleza miradi ya kijamii katika maeneo yanayozunguka migodi katika sekta mbalimbali ikiwemo kuboresha elimu, afya, miradi ya maji safi, na kuimarisha miundombinu ya barabara. Miradi hiyo imefanikisha kuleta ubora wa maisha katika jamii zinazozunguka migodi yake.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages