NEWS

Wednesday 11 October 2023

Waziri Bashungwa adokeza Serikali ilivyojipanga barabara za lami, Meneja TANROADS Mara apongezwa kwa uchapaji kazi



Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Nyamwaga, wilaya ya Tarime mkoani Mara alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo, juzi Jumatatu.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi Maalumu
-----------------------------------


WAZIRI wa Ujenzi, Innocent Bashungwa amesema Serikali imejipanga kuhakikisha wakandarasi wa ndani, wakiwemo wanaojenga barabara mkoani Mara wanalipwa kwa wakati, ili kuharakisha utekelezaji wa miradi hiyo kwa maendeleo ya wananchi. 

Aliyasema hayo juzi Jumatatu, wakati akihutubia mkutano wa hadhara katika kata ya Nyamwaga, wilaya ya Tarime mkoani Mara, alipokwenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo yenye urefu wa kilomita 25. 

“Najua utekelezaji wa mradi huu umekuwa ukisimama kutokana na kuchelewa kwa malipo, lakini niwahakikishie kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan ametoa fedha, hivyo kuanzia mwezi huu wa Oktoba tutakuwa tunalipa wakandarasi wa ndani, akiwemo anayejenga hii barabara kwa wakati ili aweze kuharakisha kazi,” alisema Waziri Bashungwa. 

Kwa upande mwingine, waziri huyo alieleza kuridhishwa na maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa na kampuni ya kizalendo ya Nyanza Road Works, kwa gharama ya shilingi bilioni 34.662 za mapato ya ndani ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. 

Mhandisi Mshauri wa ujenzi wa barabara hiyo ni kampuni ya kizalendo pia, iitwayo Advanced Engineering Solutions Ltd - ikishirikiana na JMK International Consultants Ltd, kwa gharama ya shilingi bilioni 1.563. 

Awali, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mara, Ghati Chomete alimweleza Waziri Bashungwa kuwa utekelezaji wa baadhi ya miradi ya barabara mkoani humo umekuwa ukisuasua kutokana na wakandarasi husika kucheleweshewa malipo ya fedha. 

Hata hivyo, mbunge huyo aliungana na Katibu Tawala wa Wilaya ya Tarime, Mwl Saul Mwaisenye kumpongeza Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe kwa kazi nzuri anayofanya ya kusimamia utekelezaji wa miradi ya barabara mkoani humo. “Ninampongeza Mhandisi Maribe, anafanya kazi kubwa na nzuri sana,” alisema. 


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (aliyesimama) akizungumza katika mkutano huo

Akisoma taarifa ya ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo kwa Waziri Bashungwa, Mkurugenzi wa Miradi kutoka TANROADS Makao Makuu, Mhandisi Boniface Mkumbo alisema utekelezaji wa mradi huo umefikia asilimia 30 na kwamba unatarajiwa kukamilika Januari 2024. 

Mhandisi Mkumbo alisema barabara hiyo ikikamilika itakuwa kiungo muhimu kwa wakazi wa wilaya za Tarime na Serengeti, na itarahisisha usafirishaji na biashara za mazao ya kilimo kama ndizi, mahindi na kahawa yanayozalishwa kwa wingi wilayani Tarime. 

Pia itachochea maendeleo ya sekta ya utalii kwenye Hifadhi ya Taifa Serengeti na biashara ya madini katika eneo la Nyamongo wilayani Tarime, alisema. 

Kwa mujibu wa TANROADS, mpaka sasa mradi wa ujenzi wa barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo umezalisha ajira kwa watu zaidi ya 180, kati ya hao, waajiriwa zaidi ya 170 sawa na asilimia 94.6 ni Watanzania. 

Ujenzi wa barabara hiyo ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama tawala - Chama Cha Mapinduzi (CCM), ili kuunganisha miji ya Tarime na Mugumu, Serengeti na kurahisishia wananchi usafiri. 

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya CCM Wilaya ya Tarime, Samwel Mangalaya alipopata nafasi ya kuzungumza katika mkutano huo ulimwomba Waziri Bashungwa kumfikishia Rais Samia shukrani za wana-Tarime kutokana na maendeleo ya kisekta anayowaletea. 

Viongozi wengine waliofuatana na Waziri Bashungwa katika ziara hiyo ni Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Simion Kiles, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Solomon Shati na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Wilaya ya Tarime, Marema Sollo, miongoni mwa wengine. 

Mbali na barabara ya lami Mogabiri-Nyamongo, waziri huyo pia alikagua miradi ya ujenzi wa barabara ya lami Sanzate-Natta yenye urefu wa kilomita 40 katika wilaya za Bunda na Serengeti, upanuzi na uboreshaji wa Uwanja wa Ndege Musoma, inayosimamiwa na TANROADS mkoani Mara. 

Chanzo: Gazeti la Sauti ya Mara
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages