NEWS

Friday 17 November 2023

AICT, Right to Play waombwa kuendeleza kampeni ya elimu kwa mtoto wa kike Tarime Vijijini



Na Joseph Maunya, Tarime
Mara Online News
-----------------------------


WADAU mbalimbali wameomba kampeni ya kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike - inayoendeshwa na Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play - iwe endelevu katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime (Vijijini).

Walitoa ombi hilo jana Novemba 17, 2023 wakati wa tamasha la michezo kwa wanafunzi lililoandaliwa na AICT kwa kushirikiana na shirika hilo katika viwanja vya shule za msingi Kangariani na Iramba zilizopo kata ya Itiryo wilayani Tarime, Mara.

Wanafunzi, walimu na viongozi wa vijiji na kata hiyo waliomba uhamasishaji zaidi juu ya umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike unahitajika katika eneo hilo ili kubadilisha mitazamo hasa kwa wazazi walio wengi.

“Tunaposhiriki michezo kama hii tunapata burudani na furaha, kwa hiyo nalishukuru sana shirika hili [Right to Play] na AICT, Mungu awabariki na kama inawezekana basi siku nyingine tena mrudi ili tupate elimu na burudani kama hii,” alisema Marwa Thomas, mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya msingi Iramba.

Naye mwanafunzi wa darasa la Sita katika shule ya msingi Kangariani, Lucia Mwita alisema: “Nawashukuru Right to Play kwa sababu wanatoa misaada kwa watoto wenye uhitaji kwa kuwapa vitu mbalimbali, nawaomba waje tena kutuletea matamasha kama haya.”

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kangariani, Niko Ashery alisema: “Nawashukuru sana Right to play maana mnatusaidia sana na mmewezesha mengi - siyo tu hapa Kangariani ila hata katika maeneo mengine pia tunaona, hivyo fikeni mara kwa mara kutoa hii elimu isaidie watoto wote maana hata wa kiume pia siku hizi utoro shuleni umekithiri.”

Kwa upande wake Afisa Mtendaji wa Kata (WEO) ya Itiryo, Pendo Mushi, alisema uongozi wa kata unatambua mchango mkubwa unaotolewa na Kanisa la AICT na Shirika la Right to Play katika kuhamasisha elimu kwa mtoto wa kike pamoja na kuwajengea walimu uwezo wa kusaidia kuboresha elimu na iliyo jumuishi.

WEO Pendo akizungumza
Akijibu ombi la wadau hao, Afisa Mradi kutoka AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe, Daniel Fungo aliahidi kwenda kuangalia uwezekano wa kuwa na mpango wa kuendeleza kampeni hiyo katika eneo hilo.

“Lengo la tamasha hili kwa wanafunzi ni kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike, kwa sababu jamii zetu zimeonekana kutokuwa na kipaumbele cha elimu kwa mtoto wa kike, tunalenga kuhamasisha jamii zetu zibadilike,” alisema Fungo.
Fungo akizungumza
Kanisa la AICT Dayosisi ya Mara na Ukerewe kwa kushirikiana na Shirika la Right to Play limekuwa likiendesha mradi wa kukuza elimu kwa kuwajengea walimu na wanafunzi uwezo kupitia matamasha ya michezo katika kata za Nyamwaga, Itiryo na Nyasincha wilayani Tarime.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages