NEWS

Thursday 23 November 2023

RC Mara aipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanzisha programu ya kuwajengea wafanyabiashara uwezo



Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda (katikati) na viongozi wengine wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya waafanyabiashara wanaoshiriki mafunzo ya kujengewa uwezo wa kuimarisha biashara zao, yanayofanyika mjini Tarime, leo Novemba 23, 2023. (Picha zote na Mara Online News)
--------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime

MKUU wa Mkoa (RC) wa Mara, Said Mohamed Mtanda ameipongeza Kampuni ya Barrick kwa kuanzisha programu ya kuwaendeleza wafanyabiashara kwa kuwajengea uwezo wa kuimarisha biashara zao na kushindana kitaifa na kimataifa.

Ametoa pongezi hizo leo Novemba 23, 2023 wakati akifungua mafunzo maalum ambayo ni sehemu ya programu hiyo kwa wafanyabiashara wa mkoani Mara, wakiwemo wanaotoka maeneo yanayozunguka Mgodi wa Dhahabu wa North Mara unaoendeshwa na Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Mafunzo hayo yanafanyika kwenye ukumbi wa Hoteli ya Blue Sky mjini Tarime, chini ya uratibu wa kampuni ya wazawa ya Impacten.


RC Mtanda akifungua mafunzo hayo.

Katika hotuba yake, RC Mtanda amesema mafunzo hayo ni muhimu kwani mbali na kuwaongezea uelewa, yatawawezesha wafanyabiashara hao kupata vigezo vya kunufaika na fursa mbalimbali za kibiashara ndani na nje ya mgodi wa Barrick North Mara.

“Mnaoshiriki programu hii ya mafunzo muizingatie kikamilifu ili mkidhi vigezo vya kufanya kazi na mgodi huu, najua baada ya mafunzo haya mtapata fursa za kibiashara ndani na nje ya mgodi, lakini pia mtapata elimu ya kuimarisha biashara zenu,” RC Mtanda amewambia washiriki wa mafunzo hayo.

Kiongozi huyo wa mkoa amesema Kampuni ya Barrick inastahili pongezi pia kwa kushinda Tuzo ya Mlipakodi Bora Tanzania kwa mwaka 2023, lakini pia kwa kuweza kutumia dola milioni 29 kwa ajili ya wazabuni wazawa wanaofanya biashara na mgodi wa Barrick North Mara mwaka huu.

RC Mtanda akisisitiza jambo ukumbini.

“Lakini pia kitaifa, kwa kipindi cha robo hii ya mwaka, Barrick imetumia dola milioni 51 zilizonufaisha kampuni mbalimbali zinazofanya kazi na kampuni hiyo kwa kutoa huduma mbalimbali,” ameongeza RC Mtanda.

Ametaja manufaa mengine ya mgodi huo kuwa ni pamoja na mabilioni ya shilingi yanayotolewa na Barrick chini ya mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) kwa ajili ya utekelezaji na uboreshaji wa miradi ya kijamii katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, akitolea mfano shilingi bilioni 7.3 zilizotolewa miezi michache iliyopita kugharimia utekelezaji wa miradi mbalimbali - na tayari mingi imekamilika na mingine inaendelea kutekelezwa.


Mkalimani wa Lugha ya Alama (kushoto0 akifanya kazi yake kwa washiriki wa mafunzo hayo wenye ulemavu wa kutosikia.

Aidha, RC Mtanda amesema Kampuni ya Barrick imeipatia Serikali ya Tanzania chini ya Rais Samia Suluhu Hassan shilingi bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya elimu nchini, ikiwa ni pamoja na ujenzi wa mabweni ya wasichana katika shule za sekondari za juu (high schools).

Katika hatua nyingine, RC Mtanda amewataka wazabuni wanaofanya kazi na mgodi wa Barrick North Mara kuunga mkono juhudi za kukemea na kukomesha tatizo la makundi ya watu wanaouvamia wanaojulikana kwa jina la ‘intruders’, ili waendelee kunufaika na fursa za kibiashara kutokana na uwepo wa mgodi huo.

"Waelimisheni watu waache kuvamia mgodi, msikae kimya kwa sababu ninyi pia ni wanufaika. Mgodi ukifungwa kutokana na sababu za kiusalama hata hizi dola hazitawafikia,” alisema RC Mtanda, akitolea mfano dola za Marekani milioni 29 ambazo mgodi huo umelipa kwa wazabuni wazawa kwa mwaka huu wa 2023 pekee.

Hivyo kiongozi huyo wa mkoa amesema Serikali itaendelea kushirikiana na mgodi wa Barrick North Mara na wafanyabiashara wanaofanya nao kazi katika juhudi za ulinzi wa mgodi huo na kujiinua kiuchumi.

RC Mtanda ametumia nafasi hiyo pia kuwapatia wafanyabiashara wanaoshiriki mafunzo hayo zawadi ya vitabu 10 vyenye mwongozo wa fursa za uwekezaji zilizopo katika mkoa wa Mara.


RC Mtanda akimkabidhi Mwalimu Mwita kutoka Professor Mwera Foundation kitabu chenye mwongozo wa fursa za uwekezaji katika mkoa wa Mara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele akizungumza kabla ya kumkaribisha RC Mtanda, amesisitiza kuwa mafunzo hayo yatawafungulia wafanyabiashara hao milango ya kunufaika na fursa nyingi za kibiashara hata nje ya Tanzania.

Awali, Kaimu Meneja wa Idara ya Mahusiano Mgodi wa Barrick North Mara, Hermence Christopher amesema mafunzo hayo yanahudhuriwa na wafanyabiashara wenye kampuni zikiwemo zinazofanya kazi na mgodi huo, na kwamba mpango huo ni mwendelezo wa jitahada wanazofanya kuwajengea wafanyabisahara wazawa uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mnyororo wa uchumi wa madini.

“Sera ya Local Content inatutaka kuwajengea Watanzania uwezo wa kushiriki vizuri kwenye shughuli zetu. Hivyo ili kuhakikisha kuwa wanashiriki kwenye mnyororo wa uchimbaji wa madini, tumekuja na Local Business Development Programe (Programu ya Kuendeleza Wafanyabiashara),” amesema Hermance ambaye amemwakilisha Meneja Mkuu wa mgodi huo, Apolinary Lyambiko.


Hermence akiwaeleza wafanyabiashara hao umuhimu wa mafunzo hayo.

Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo wameishukuru Kampuni ya Barrick, na kuahidi kuyazingatia kwani ni fursa muhimu kwao. “Tumefurahi sana kwa ajili ya programu hii, tunategemea mgodi utatufanyia mambo mengi mazuri,” amesema Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Range.


Mkurugenzi wa Kampuni ya RIN, Isack Range (kushoto) akizungumza mbele ya RC Mtanda (wa tatu kushoto) na viongozi wengine.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Miradi wa Kampuni ya Impacten inayoratibu mafunzo hayo, Winfrida Minja, yataendelea kwa awamu hadi Februari 2024.

Kampuni ya Barrick kupitia Mgodi wake wa North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime, imeandaa programu hiyo baada ya kubaini kuwa kampuni nyingi za kibiashara mkoani Mara haziwezi kushindana kwa tija na zinazotoka mikoa mingine na nje ya Tanzania, lakini pia zimekuwa haziendeshwi kimkakati ili kuzalisha faida, na kwa kiwango kikubwa hazikidhi vigezo, masharti na kanuni za Barrick na Serikali.

Mafunzo hayo yanaendeshwa na washauri wabobezi wa masuala ya kibiashara kutoka sekta ya umma na binafsi, ambapo yanatarajiwa kuwaongezea wafanyabiashara hao ujuzi, maarifa, mbinu na uwezo wa kubaini fursa mpya za kibiashara ndani na nje ya nchi ili kuweza kufikia malengo yao - wakizingatia vigezo, masharti, sheria na kanuni za Serikali na Kampuni ya Barrick.

Kimsingi yanafanyika chini ya mpango wa Uendelezaji Biashara North Mara 2023, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Sheria ndogo ya The Mining (Local Content) Regulations ya Mwaka 2018.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages