NEWS

Friday 8 December 2023

Maafa Hanang: Chatanda alivyomwaga chozi baada ya kuona mama aliyeokolewa mafuriko amejifungua mtoto

Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mary Chatanda (katikati) akilia kwa uchungu baada ya kumtembelea mama aliyeokolewa kwenye maafa ya mafuriko wilayani Hanang akiwa amejifungua mtoto wa kiume salama.


NA MWANDISHI WETU, Hanang

---------------------------------------

Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Taifa, Mary Chatanda na msafara alioambata nao wamejikuta katika simanzi kubwa mara baada ya kumuona mama aliyejifungua saa chache baada ya kuokolewa kwenye tope lililomsomba mita kadhaa.

 

Akizungumza wakati alipomtembelea mwanamke huyo juzi katika Kituo cha Afya Gendabi wilayani Hanang, mahali yalipotokea maafa ya mafuriko na maporomoko ya tope kutoka Mlima Hanang.

 

"Nimeshindwa kujizuia mimi kama mama nikajikuta nalia kwa uchungu kuona mwanamama huyu ambaye alisombwa na tope na kuweza kuokolewa kwenye tope hilo na kufikishwa hospitali masaa mawili baadaye akajifungua salama mtoto wa kiume,” alisema Chatanda na kuendelea:

 

“Kwa kweli nimelia uchungu baada ya kusikiliza simulizi za mama huyu namna alivyohangaika kuokoa watoto wake wawili na huku mjamzito wa miezi tisa, hakika hakuna kama mama. Namshukuru sana Mungu kutenda maajabu na kumwezesha mama huyu kujifungua salama na mtoto yupo salama na ameitwa Mussa." 

 

Aidha, Mwenyekiti huyo wa UWT Taifa, alisema jumuiya hiyo ya chama tawala - CCM itafanya jitihada kuhakikisha wanamuimarishia mahitaji mama huyo ambaye kwa sasa na familia yake wanalala hospitalini kutokana na makazi yao kuharibiwa na mafuriko yaliyoambatana na tope.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages