NEWS

Friday, 1 December 2023

Maadhimisho Siku ya Ukimwi Duniani 2023: Mgodi wa Barrick North Mara wapongezwa, DC Tarime awataka watu kuepuka ngono zembe



Wananchi wakiwemo wanafunzi wakiwa kwenye foleni ya kupata huduma za kupima afya wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kiwilaya katika viwanja vya Nyamwaga wilayani Tarime, Mara leo Desemba 1, 2023.
------------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
---------------------------------------


Serikali wilayani Tarime imeupongeza Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara kwa kushiriki na kuwezesha shughuli mbalimbali za maadhimisho ya Siku ya Ukimwi mwaka huu wa 2023.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kiwilaya leo Desemba 1, 2023 katika viwanja vya Nyamwaga, mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Wilaya (DC) ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele.


Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele (katikati) akisikiliza maelezo ya huduma za afya katika mojawapo ya mabanda kwenye maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kiwilaya kwenye viwanja vya Nyamwaga leo.
-------------------------------------------------------

Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo imeutaja mgodi wa Barrick North Mara kama mdau mkubwa aliyechangia kwa hali na mali kufanikisha maadhimisho hayo.

“Barrick wameshiriki kufadhili na kuratibu shughuli mbalimbali za maadhimisho haya, lakini pia wanashirikiana na Idara ya Afya katika utoaji wa elimu ya kujikinga na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU),” amesema Mratibu wa Ukimwi, Dkt Joel Mubala.


Mratibu wa Ukimwi, Dkt Joel Mubala akisoma taarifa ya utekelezaji wa afua za Ukimwi katika maadhimisho hayo.

Awali, Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi amesema upimaji wa VVU ni moja ya kampeni zinazozingatiwa kwa wafanyakazi wa mgodi huo. “Afya bora ni mtaji muhimu katika shughuli zetu,” amesema.


Meneja Mahusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi akizungumza wakati wa maadhimisho hayo.

Katika hotuba yake, DC Mntenjele ameupongeza mgodi huo kutokana na mchango wake mkubwa kwenye kampeni za kutoa elimu ya kujikinga na VVU, pamoja na maambukizi mengine kwa wafanyakazi wake na jamii inayouzunguka.

“Tumeona foleni kubwa ya watu waliojitokeza kupata huduma za kupima afya zao katika maadhimisho haya, hii yote ni kutokana na hamasa kubwa iliyotolewa na wadau,” amesema DC Mntenjele na kuwaomba wadau mbalimbali kuendelea kuiunga mkono Serikali katika jitihada za kupunguza maambukizi ya VVU na uboreshaji wa huduma nyingine za afya kwa wananchi.



Aidha, Mkuu huyo wa wilaya ameitaka jamii kuepuka vitendo vinavyochangia maambukizi ya VVU kama vile ngono zembe, ukeketaji na tohara zisizo salama, mila za utakasaji na nyumba ntobhu kwani zina madhara makubwa ya kiafya, kiuchumi na kijamii.

“Mila hizi ikiwemo ya ukeketaji zimepitwa na wakati na zina madhara makubwa, ikiwa ni pamoja na watu kupoteza uhai, kupungua kwa nguvu kazi na pato la familia na taifa, lakini pia kuathiri uwekezaji na maendeleo katika jamii,” amesema.


DC Mntenjele akihutubia wananchi katika maadhimisho hayo.

Mkuu huyo wa wilaya ametumia nafasi hiyo pia kuupongeza Mgodi wa Barrick North Mara kwa jitihada zake za kuibua miradi ya kuwezesha vijana kiuchumi katika vijiji vinavyouzunguka.

“Endeleeni na jitihada hizi kwa sababu miradi hii itasaidia kupunguza wimbi la uvamizi mgodini - jambo ambalo siyo la tija,” amesema DC Mntenjele.

Katika maadhimisho hayo, wananchi wamepata huduma mbalimbali za afya bila malipo, ikiwemo ushauri nasaha na kupima VVU, uchunguzi wa kifua kikuu, upimaji wa homa ya ini, macho, chanjo ya UVIKO 19, tohara salama na uchangiaji damu kwa hiari.


Huduma za upimaji zikiendelea kwenye viwanja vya Nyamwaga.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Ukimwi, Dkt Mubala, kiwango cha maambukizi ya VVU katika wilaya ya Tarime kwa waliopimwa kimepungua kutoka asilimia 2 mwaka 2022 hadi asilimia 1.7 kufikia Oktoba 2023.

Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa Desemba 1 kila mwaka. Kaulimbiu ya maadhimisho hayo mwaka huu wa 2023 inasema: “Jamii Iongoze Kutokomeza Ukimwi”. Na ya kiwilaya inasema: “Tarime Bila Maambukizi ‘Mapya’ ya VVU Inawezekana”.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages