NEWS

Friday 8 December 2023

Taa za barabarani zahujumiwa Tarime MjiniNguzo ya iliyovunjwa na kunyofolewa betri na taa ya barabarani eneo la TTC mjini Tarime usiku wa kuamkia jana Ijumaa. (Picha na Sauti ya Mara)
-----------------------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Tarime
-----------------------------------------------

Kuna hatari ya kuirejesha mji wa Tarime kwenye zama za giza ikiwa hatua za makusudi hazitachukuliwa kudhibiti wimbi la vitendo vya uharibifu na wizi wa taa za barabarani. 

Kwa sasa usalama wa taa zilizowekwa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mara katika senta za miji na vijiji vyenye barabra ya lami uko hatarini. 

Mfano usiku wa kuamkia jana Ijumaa watu ambao hawajajulikana walivunja nguzo ya chuma na kuiba taa na betri yake katika barabara ya Tarime-Musoma-Mwanza eneo la Chuo cha Ualimu Tarime (TTC). 

Sauti ya Mara ilifika eneo la tukio na kushuhudia nguzo hiyo imelala chini ikiwa imenyofolewa taa na betri baada ya nati zilizokuwa zimeifunga kufunguliwa. 

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Kipolisi Tarime Rorya, ACP Mark Njera hakupatikana haraka kwa ajili ya kuzungumzia tukio hilo. 

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mara, Mhandisi Vedastus Maribe alizungumanza na gazeti hili kwa njia ya simu na kuonya kuwa watakaokamatwa kuhusiana na uhalifu huo watashtakiwa kwa makosa ya uhujumu uchumi. 

Aidha, Mhandisi Maribe alitumia nafasi hiyo pia kutoa wito wa kuwataka wakazi wa Tarime kuwa walinzi wa usalama wa taa za barabarani kwa manufaa yao na taifa kwa ujumla. 

Uwekaji wa taa mpya za barabarani kwenye senta za miji na vijiji vya Halmashauri ya Mji wa Tarime ulitekelezwa na Serikali kupitia TANROADS Mkoa wa Mara miezi michache iliyopita. 

Wakazi wa wilaya ya Tarime waliipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, wakisema taa hizo zimesaidia pia kuimarisha ulinzi na usalama na hivyo kupunguza matukio ya vibaka ambao wamekuwa wakivamia na kupora mali za watu wakiwemo wasafiri nyakati za usiku. 

Lakini pia taa hizo zinatajwa kuchochea shughuli za kibiashara na ukuaji wa uchumi kutokana na wananchi sasa hivi kufanya biashara hadi usiku - tofauti na siku za nyuma. 

Kwa mujibu wa Mhandisi Maribe, taa hizo zinatumia umeme wa jua (solar) na zina uwezo wa kujiwasha kuanzia saa moja jioni hadi asubuhi kila siku. 

Wilaya ambazo tayari zimenufaika na mpango huo wa kuwekewa taa za barabarani katika mkoa wa Mara ni Bunda, Musoma, Rorya na Tarime.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages