NEWS

Tuesday 30 January 2024

Kuji sasa rasmi Kamishna wa Uhifadhi TANAPA, Waziri Kairuki aongoza hafla ya uapisho wakeKamishna mpya wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji.
-------------------------------------------


Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki (kulia) akiongoza hafla ya uapisho wa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA, Juma Kuji jijini Arusha jana.
-----------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Arusha
---------------------------------------


KAMISHNA mpya wa Uhifadhi (CC) wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Juma Kuji amekula kiapo cha utii, katika hafla iliyoongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki makao makuu ya shirika hilo jijini Arusha jana Jumatatu.

Akizungumza baada ya uapisho huo, Waziri Kairuki alimwagiza CC Kuji kusimamia na kuhakikisha ulinzi wa maliasili unaimarishwa na doria zinafanyika wakati wote kukabili vitendo visivyofaa vya ujangili Hifadhi za Taifa, ikiwemo uchungaji mifugo na uchimbaji wa madini.“Endelea kuhakikisha kuwa hifadhi zinaendelea kuimarika, kukusanya mapato, lakini hifadhi zingine ziendelee kufanya vizuri kama ambavyo Serengeti inafanya vizuri. Nunueni vitendea kazi na kuboresha maslahi ya watumishi, pamoja na kuendelea kujikita kutangaza utalii kwa kushirikiana na taasisi zingine kama TTB,” aliongeza waziri huyo mwenye dhamana ya maliasili na utalii nchini.

Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt Hassan Abbas alisisitiza umuhimu wa viongozi na wafanyakazi wa TANAPA kufanya kazi kama timu.“Nafasi hizi zinakuja na majukumu yake, “team work” ni muhimu sana. TANAPA ni taasisi kubwa sana nchini na duniani, shirikianeni, na sisi wizara tutakuwa tayari kushirikiana na wewe. Mtegemee Mwenyezi Mungu katika majukumu yako,” alisema Dkt Abass.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA, Jenerali Mstaafu George Waitara alimpongeza Kuji kwa kuteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa shirika hilo la umma.“Binafsi sina mashaka na uzoefu wako ndani shirika wa miaka 33, ni matumaini yangu uzoefu huo utautumia katika kukuza uhifadhi na utalii na kuendelea kufanya vizuri katika ngazi za kimataifa,” alisema Jenerali Mtaafu Waitara.

Kwa upande wake CC Kuji aliahidi ushirikiano na watumishi wote ili kuhakikisha wanalinda urithi wa maliasili zilizopo nchini kwa kutekeleza majukumu yao kwa bidii na nidhamu.“Awali ya yote namshukuru Mungu kwa tukio hili la kuvishwa vyeo, pili nimshukuru Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuniteua kuwa Kaimu Kamishna na baadaye kuwa Kamishna wa Uhifadhi wa TANAPA,” alisema CC Kuji na kusisitiza kuwa ushirikiano kwa watumishi utawawezesha kufikia adhma ya serikali ya kuanzisha shirika hilo.

Aliongeza: “Mimi na watumishi wenzangu kwa kushirikiana na Bodi ya Wadhamini tutaendelea kusimamia kikamilifu maeneo ya hifadhi wakati wote, tutajitahidi kutumia taaluma, uzoefu, busara na kumtanguliza Mungu katika kuhakikisha rasilimali zote zilizopo katika Hifadhi za Taifa zinahifadhiwa kikamilifu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages