Rais Dkt Samia Suluhu Hassan
----------------------------------------
NA MWANDISHI WETU
----------------------------------
RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan, jana alihutubia Taifa pamoja na kutoa salamu za mwaka mpya 2024 kupitia vyombo mbalimbali vya habari.
Katika hotuba yake, Rais Samia pamoja na mambo mengine, aligusia jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali mwaka 2023 katika kuboresha huduma za kijamii nchini.
Alisema Serikali ya Awamu ya Sita anayoiongoza inaendelea kuongeza juhudi za kuboresha maslahi ya watumishi na maisha ya wananchi kwa ujumla katika nyanja za kijamii na kiuchumi.
Aidha, Mkuu huyo wa nchi alitumia nafasi hiyo pia kuwahimiza wananchi kulinda vyanzo vya maji na kulipa bili za huduma ya maji kwa wakati.
Kuhusu utunzaji wa mazingira, Rais Samia aliendelea kuzisisitiza halmashauri zote nchini kila moja kuhakikisha inapanda miti milioni 1.5 kwa mwaka.
Akizungumzia mfumuko wa bei za bidhaa nchini alisema: "Tumeendelea kudhibiti mfumuko wa bei ambao katika kipindi cha Januari - Novemba 2023 ulipungua hadi wastani wa asilimia 3.9, ikilinganishwa na wastani wa asilimia 4.3 kipindi kama hicho mwaka 2022."
Kwa upande wa kilimo Rais alisema: “Tumeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 751 mwaka jana hadi shilingi bilioni 970 mwaka huu, sawa na ongezeko la asilimia 29. Sababu yetu ni kuchochea kiwango cha ukuaji wa sekta ya kilimo kufikia asilimia 10 kwa mwaka - ifikapo mwaka 2030.”
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Tunakuhabarisha Ukweli kwa Weledi
No comments:
Post a Comment