NEWS

Monday 1 January 2024

TCCIA yaahidi kumsaidia Rais Samia kupaisha uchumi wa Taifa



Makamu wa Rais wa TCCIA (Biashara), Boniface Ndengo akizungumza na waandishi wa habari mjini Musoma leo Januari 1, 2024.
-----------------------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Musoma
--------------------------------------


CHEMBA ya Biashara, Viwanda na Kilimo Tanzania (TCCIA) imeahidi kumsaidia Rais Dkt Samia Suluhu Hassan katika jitihada za kukuza uchumi wa Taifa kupitia sekta binafsi.

Imefafanua kuwa ili kufikia lengo la kukuza uchumi wa Tanzania kutoka asilimia nane mwaka 2023 hadi asilimia 20 mwaka 2024, unahitajika ushirikiano wa karibu kati ya sekta binafsi na Serikali.

Kauli hiyo imetolewa na Makamu wa Rais wa TCCIA upande wa Biashara, Boniface Ndengo katika mkutano na waandishi wa Habari mjini Musoma leo Januari 1, 2024.

Ndengo ambaye amemwakilisha Rais wa TCCIA, Vicent Minja katika mkutano huo, alikuwa akitoa salamu za wafanyabiashara na wadau wa sekta binafsi kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan.

"Tunamshukuru Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa namna anavyotekeleza majukumu yake ya kuwaletea wananchi maendeleo. TCCIA kama chemba ya wafanyabiashara tunaihidi kumpa ushirikiano wote ili kuhakikisha malengo kusudiwa ya Taifa yanafikiwa,” amesema Ndengo.

Amesema kwamba wakati Rais Samia akilihutubia Taifa na kutoa salamu za mwaka mpya jana Desemba 31, 2023, alitaja mipango ya Serikali ya kuwaletea wananchi maendeleo na mwongozo unaopaswa kufuatwa.

"Kwa niaba ya Rais wa TCCIA na wafanyabiashara wote, tunaahidi tena kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia ili kufikisha Taifa mahala sahihi,” amesema Ndengo ambaye pia ni Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mara.

Amesema sekta binafsi inahamasisha masuala ya uwekezaji kwa wafanyabiashara wakubwa kwa ajili ya kuwekeza katika shughuli za kiuchumi.

Kwa mujibu wa Ndengo, uwekezaji unakuza uchumi wa nchi na kusaidia mambo mengine ya Serikali kuendelea kufanyika kwa manufaa ya umma.

Hivyo ametumia nafasi hiyo kumhakikishia Rais Samia kuwa wafanyabiashara watahimizwa kulipa kodi kwa wakati ili Serikali iweze kutekeleza miradi ya kuwahudumia wananchi.

Amesema kutolipa kodi kwa wakati ni kushindwa kutekeleza wajibu, hivyo TCCIA itaendelea kuwahimiza wafanyabiashara kutambua umuhimu wa kulipa kodi.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages