NEWS

Sunday 14 January 2024

Wananchi: Mahusiano kati ya mgodi wa Barrick North Mara na jamii yanaendelea kuwa mazuri



Lori likiwa kazini katika Mgodi wa Dhahabu wa North Mara
---------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
------------------------------------------


WANANCHI mbalimbali wameeleza kuridhishwa na maendeleo ya uboreshaji wa mahusiano kati ya Mgodi wa Dhahabu wa North Mara na jamii inayouzunguka.

Mgodi huo ambao upo Nyamongo wilayani Tarime, Mara, unaendeshwa na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Wakitoa maoni na tathmini yao katika mazungumzo na Sauti ya Mara kwa nyakati tofauti wiki iliyopita, wakazi wa maeneo jirani na mgodi huo, walisema mahusiano na jamii inayouzunguka yanazidi kuimarika.

“Mimi kama mdau wa jamii, ninaona mahusiano yanaimarika pamoja na kwamba kwa tabia ya kibinadamu huwezi kumridhisha kila mtu. Ninaona kwamba kwa kipindi cha hivi karibuni, mahusiano yanaimarika.

“Tukianzia kwenye nyanja ya uchumi, ni kwamba mgodi umeweza kufanikiwa kusaidia jamii za hapa kupitia ‘local content’- kwa maana ya kuruhusu wazawa wanaoishi katika vijiji vinavyozunguka mgodi kufungua kampuni mbalimbali na kufanya nao biashara.

“Kwa sasa hivi nadhani kuna kampuni zaidi ya 80 ambazo zinafanya biashara na mgodi wa North Mara - kwa maana ya Barrick wenyewe, lakini pia kwa ile Kampuni Swala Solution ambayo wameipatia mamlaka ya kufanya ‘screening’ ya kupata bidhaa,” anasema Nicodemus Keraryo, mkazi wa kata ya Matongo, Nyamongo.

Keraryo ambaye ni msomi mwenye elimu ya chuo kikuu na Mkurugenzi Mtendaji wa Timbo Contractor Manpower and General Supply Co. Ltd, anafafanua kuwa baadhi ya kampuni za wazawa zimesajiliwa na mgodi moja kwa moja, na nyingine zimesajiliwa na Swala Solution kwa ajili ya huduma mbalimbali za mgodini. “Kwa hiyo kuna ongezeko kubwa sana la kampuni za wazawa zinazofanya kazi na mgodi. Hilo ni jambo la kuipongeza sana Kampuni ya Barrick,” anasema.


Nicodemus Keraryo
Hata ongezeko la biashara na mzunguko wa fedha katika mji wa Nyamongo - vinavyochochewa na uwepo wa mgodi huo, Keraryo anasema ni miongoni mwa vitu vinavyochangia kuboresha mahusiano ya pande zote mbili, akijitolea mfano wa Kampuni yake ya Timbo.

“Mji wa Nyamongo unakua kwa kiasi kubwa sana. Kupitia mzunguko wa fedha na uwezo wa mgodi - kwa maana ya haya mahusiano mazuri, jamii yetu inaendelea kuboreka kimaisha.

“Na ikumbukwe kwamba katika kampuni hizi za wazawa tumeajiri watu mbalimbali kutoka vijiji vilivyo jirani na mgodi, na hii inasababisha mzunguko wa fedha Nyamongo unakuwa mkubwa. Kwa hiyo hayo ni mahusiano mema ambayo mgodi umetengeneza na wazawa wa hapa,” anaongeza Keraryo.

Anaendelea: “Jambo lingine, nimeona Barrick wanajitahidi sana kwenye suala la ajira, tunaona vijana wengi wanaajiriwa katika mgodi huu, na wazawa wa hapa ndio wanapewa kipaumbele cha kwanza. Kwa hiyo tunaona utaratibu huo unasaidia kuimarisha mahusiano na jamii.”

Anataja kingine kinachochasaidia kuboresha mahusiano kuwa ni miradi ya kijamii inayotekelezwa kutokana na mabilioni ya fedha zinazotolewa na mgodi wa Barrick North Mara kupitia mpango wake wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR).

“Kwenye huduma za jamii, tunaona hata kipindi hiki kuna mradi mkubwa wa maji Nyangoto ambao unahudumia vijiji vya kata ya Matongo. Hivyo kwa kweli wananchi tunaupongeza mgodi kwa nyanja hiyo pia,” anasema Keraryo na kuongeza:

“Kitu kingine kinachoonesha kukua kwa mahusiano kati ya mgodi wa North Mara na jamii ukilinganisha na kipindi cha nyuma, ni kupungua kwa vitendo vya uhalifu katika mji wa Nyamongo, japokuwa kule mgodini bado vitendo vya intrusion (uvamizi) havijaisha, na hili tatizo linahitaji ushirikiano wa viongozi wa mgodi na wananchi kulitafutia ufumbuzi.”

Keraryo anashauri mgodi kupitia idara yake ya mahusiano kuongeza nguvu ya kushirikiana na viongozi wa kijamii wakiwemo wenyeviti wa vijiji na madiwani kuelimisha wananchi kutambua kuwa mgodi huo ni sehemu ya maisha yao, hivyo unahitaji kulindwa.

Pia katika nyanja ya kuboresha mahusiano, pande zote [mgodi na jamii] zishirikiane kuangalia namna nzuri ya kuweza kuandaa ‘mgodi’ mwingine wa baadaye, ili baada ya huo wa North Mara kufikia ukomo, jamii inayouzunguka iwe na vyanzo vingine vya mapato.

“Mfano, vijiji vyetu vinapakana na bonde la mto Mara, mgodi unaweza kuwezesha jamii yetu kulitumika kwa kilimo cha miwa - watu wakapata ajira kuanzia shambani hadi kuuza na kupaki miwa, kuendesha magari ya mradi na hata kupata fursa za kujenga nyumba za makazi ya watu wanaofanya kazi kwenye kiwanda cha kukamua miwa.

“Kwa hiyo, hata baada ya mgodi kufungwa wananchi wa huku tutakuwa na ‘mgodi mwingine’ ambao utaifanya Nyamongo isiwe mahame, tutakuwa na chanzo kingine cha ajira na mapato, na hilo pia ni suala la kimahusiano.

“Lakini pia ninaona umuhimu wa viongozi wa mgodi na wananchi kuja na mpango maalum wa kuelimisha jamii yetu jamii kupenda miradi ya kijamii na kiuchumi tunayoanzishiwa.

“Mfano pale kijijini Matongo kuna mradi mkubwa wa kilimo cha mboga mboga ambao ulioanzishwa kwa ufadhili mkubwa wa Kampuni ya Barrick kwa ajili ya vijana kujikwamua kiuchumi, lakini naona vijana hawajauchangamkia kwa wingi.

“Kwa hiyo, jamii iangalie kwamba mgodi hauwezi kuwepo kila siku, ipo siku utaisha. Tunataka mgodi ukiisha jamii iwe na sehemu ya kujipatia kipato na kuendeleza maisha. Jambo hili ni muhimu kuzingatiwa ili ikitokea mgodi umefungwa, tusiwe kama tumeshtushwa halafu tukakosa cha kufanya,” anasema Keraryo.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyamongo, Mwl Charles Paschal Gamba naye anakiri kuwa mahusiano kati ya mgodi wa Barrick North Mara na jamii inayouzunguka yanazidi kuimarika.



Mwl Gamba
“Kwa sasa hivi mahusiano yameimarika sana kutokana na elimu inayotolewa, lakini pia kutokana na faida ambazo wananchi wa huku wanazipata kupitia mgodi huu; kama vile miradi ya maji, elimu na kadhalika. Mfano pale shuleni kwangu mgodi umetujengea mabweni na uzio wa ukuta na nyaya.

“Lakini pia katika kata yetu ya Matongo, mgodi huo huo wa North Mara kupitia mpango wake wa CSR, umetujengea shule mbili za sekondari, moja tayari imefunguliwa na nyingine inakaribia kufunguliwa katika kijiji cha Mjini Kati.

“Kwa hiyo watu wanaona, hata juzi nilikuwa kwenye mkutano wa kata - watu wamehamasika sana, kwa ujumla mahusiano yanazidi kuwa mazuri, wananchi wanaona mgodi unawasaidia sana kuliko zamani,” anasema Mwl Gamba.

Kuhusu vitendo vya uvamizi mgodini, anasema mgodi na jamii inayouzunguka ikishirikiana kwa dhamira ya dhati inaweza kukomesha kuvikomesha kwa kuwa vijana wengi wanaojihusisha na uhalifu huo wanatoka nje ya vijiji vinavyozunguka. “Wakati mwingine unaweza kukuta katika wavamizi 10, Mnyamongo ni mmoja na tisa wanaobaki ni kutoka nje ya Nyamongo,” anasisitiza.

Hivyo Mwl Gamba anashauri elimu iendelee kutolewa katika kila kijiji kupitia mikutano ya hadhara, sambamba na kuongeza nafasi za ajira za mgodini kwa wakazi wa vijiji jirani.

Kwa upande mwingine, Mwl Gamba anasema vilabu vya Marafiki wa North Mara (Friends of North Mara) vilivyoanzishwa kwenye shule mbalimbali za maeneo yaliyo jirani na mgodi huo zitasaidia kuboresha zaidi mahusiano baina ya pande zote mbili.

“Hivi vilabu (Friends of North Mara ) vitaboresha sana mahusiano kati ya mgodi na jamii inayouzunguka, kwa sababu tunajenga kizazi cha kutambua manufaa ya mgodi. Zamani jamii ya huku iliona mgodi ni adui wa maisha yao, lakini sasa hivi hata watoto wanasema ‘kumbe una manufaa, tunajengewa mabweni, tunajengwe shule, tunapata maji, kwanini tuwe na ugomvi na mgodi huu’.

“Lakini pia siku hizi huku watoto wanahamasishwa sana kusoma kwa bidii ili waweze kupata ajira za mgodini zenye mnyororo mzuri wa maisha kuliko short cut (njia ya mkato). Hivyo miaka 10 ijayo jamii yenyewe itakuwa inakatazana kuhujumu mgodi huu ili iendelee kunufaika nao,” anasema Mwl Gamba.

Diwani wa Viti Maalum Tarafa ya Ingwe katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Felister Range yeye anataja mashindano ya soka ya Mahusiano Cup yanayodhaminiwa na Barrick North Mara kuwa ni miongoni mwa mikakati yenye matokeo chanya katika kuboresha mahusiano ya mgodi huo na jamii inayouzunguka.


Diwani Felister Range
“Haya mashindano yanafanyika kila mwaka na mgodi unawapa washindi zawadi, wanafanya vizuri. Pia Barrick wanataka kujenga uwanja wa kisasa wa mpira katika kata ya Matongo, na mimi niko kwenye kamati ya michezo, hili nalo litasaidia kuboresha zaidi mahusiano maana litaibua vipaji vya michezo na kutengeneza ajira kwa vijana wetu,” anasema Diwani Felister.

Naye Katibu wa Wazee wa Mila wa koo 12 za kabila la Wakurya wilayani Tarime, Mwita Nyasibora anasema wanaridhishwa na jitihada mbalimbali zinazofanywa na mgodi wa Barrick North Mara kuboresha mahusiano na jamii inayouzunguka, ikiwemo kupitia ufadhili wa miradi mbalimbali ya kijamii.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages