NEWS

Tuesday 13 February 2024

Dar watoa heshima za mwisho kumuaga Lowassa, Makamu wa Rais Dkt Mpango na vigogo wengine wammiminia sifaAskari wakiwa wamebeba mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu Edward Lowassa (pichani kushoto) kwenye viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam ulipoagwa leo.
---------------------------------------------

Na Mwandishi wa
Mara Online News
------------------------------


MAMIA ya wananchi wakiwemo viongozi mbalimbali wa serikali, dini na vyama vya siasa wamejitokeza kutoa heshima za mwisho na kuaga mwili wa Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa, katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam leo.

Wameongozwa na Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango aliyemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan katika shughuli hiyo.

Dkt Mpango ametoa pole kwa familia na ndugu wa marehemu, marafiki na Watanzania ujumla kutokana na msiba huo.


Makamu wa Rais Dkt Mpango akizungumza
--------------------------------------------
Makamu wa Rais amesema Lowassa alikuwa “mtoto mahiri wa mama Tanzania” ambaye alijitoa kwa dhati kulitumikia taifa kwa moyo wake wote.

“Mheshimiwa Lowassa alitumia vema karama ambazo alijaaliwa na Mwenyezi Mungu kuwatumikia Watanzania katika nyadhifa mbalimbali. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa zawadi ya Mheshimiwa Lowassa. Tunathamini uzalendo na mchango wake mkubwa kwa maendeleo ya nchi yetu,” amesema.

Aidha, amewataka Watanzania wanapomuaga Lowassa wajikumbushe wajibu wa kila mmoja kwa nchi yetu na kuyaishi kwa vitendo mambo yote mazuri waliyojifunza kutoka kwenye maisha yake.


Waziri Nape Nnauye akiaga mwili
--------------------------------------------
“Maisha ya Mheshimiwa Edward Lowassa yametuachia sisi Watanzania mafunzo mengi. Alikuwa mchapakazi hodari katika utumishi ndani ya Chama Cha Mapinduzi na katika utumishi wa umma, lakini hata katika shughuli zake binafsi kama vile ufugaji.

“Kwa hiyo inatupasa Watanzania tumuenzi kwa kuendelea kuchapa kazi ili kuboresha maisha yetu na kuchangia katika ujenzi wa taifa.

“Lowassa [alipokuwa Waziri Mkuu] aliweka juhudi kubwa kubuni miradi ya maji ili yawafikie Watanzania wengi katika maeneo yenye uhaba, ukiwemo mradi wa kutoa maji Ziwa Victoria kwenda Shinyanga, Tabora na sasa umefika Singida kuelekea Dodoma, ni kazi dhahiri na alama aliyotuachia Mheshimiwa Lowassa.

“Kwa hiyo, viongozi wa leo na kesho mnapaswa kumuiga Mheshimiwa Edward Lowassa kuwa na uthubutu wa kubuni mambo makubwa kwa maendeleo ya nchi yetu.

“Mheshimiwa Lowassa aliipenda sana familia yake na ndugu zake, na hasa aliwasaidia sana wasio na uwezo, na kwa hiyo inatupasa nasi tuige mfano huo mzuri katika malezi ya familia na jamii inayotuzunguka.

“Mheshimiwa Lowassa alikuwa na bidii katika kumwabudu Mwenyezi Mungu, alikuwa mshirika hodari akisali mara nyingi katika Usharika wake wa KKKT, sasa mfano huu utukumbushe kuwa kumcha Mungu ndiyo chanzo cha maarifa na msingi wa mafanikio katika familia na utumishi wa umma.

“Mheshimiwa Rais na Serikali nzima tunaiombea familia yake [Lowassa] faraja kutoka kwa Mungu… tuiombee roho yake ipate pumziko la amani mbinguni,” amesema Makamu war ais Dkt Mpango.


Rais Mstaafu Kikwete akizungumza wakati wa kuaga mwili wa Lowassa kwenye viwanja vya Karimjee
------------------------------------------
Viongozi wengine waliopata nafasi ya kuzungumza na kummiminia Lowassa sifa ni kama ifuatavyo:

“Lowassa amefanya makubwa kwa taifa. Neno ninaloweza kusema ni shukrani nyingi kwake, na kikubwa kwa sasa ni kumwombea kwa Mwenyezi Mungu,” amesema Rais Mstaafu wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete.

“Edward Lowassa alipenda kujifunza wakati wote, hamu yake kwa Watanzania alitamani nchi nzima iwe na maji,” amesema Rais Mstaafu wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein.

“Jambo kubwa Edward alikuwa na imani ya kulitumikia taifa, pamoja na changamoto nyingi alizopitia katika siasa,” amesema Jaji Mstaafu na Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba.

“Edward Lowassa alifanya mazuri serikalini, alifanya kazi nzuri kwenye chama na jamii kwa ujumla. Watanzania hatutaweza kumsahau kwa uchapakazi wake uliotukuka,” amesema Waziri Mkuu Mstaafu, Frederick Sumaye.


Mtoto wa Lowassa, Fred Lowassa akizungumza wakati wa kuaga mwili wa baba yake kwenye viwanja vya Karimjee.
-------------------------------------------
“Msiba huu siyo wa ukoo wa Lowassa tu, bali watoto wanaosoma shule za kata wanaomboleza, wananchi wanaokunywa maji kutoka Ziwa Victoria wanaomboleza, wanafunzi wanaosoma Chuo Kikuu Dodoma (UDOM) wanaomboleza na wananchi wengine wengi wanaomboleza,” amesema mtoto wa Edward Lowassa, Fred Lowassa.

Waziri Mkuu Mstaafu, Edward Ngoyai Lowassa alifariki dunia Februari 10, 2024 jijini Dar es Salaam akiwa katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete alipokuwa akiendelea kupata matibabu ya maradhi ya mapafu na shinikizo la damu.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages