NEWS

Wednesday 21 February 2024

Kamati ya Bunge yavutiwa na utendaji mgodi wa Barrick North Mara



Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo David (katikati) akizungumza kwenye kikao cha kamati hiyo wakati wa ziara yao ya kikazi katika Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara jana.
----------------------------------------------

NA WAANDISHI WETU, Nyamongo
--------------------------------------------------

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini imeipongeza Kampuni ya Barrick Gold kwa kubadilisha mazingira ya mgodi wa North Mara kuwa mazuri zaidi ukilinganisha na miaka ya nyuma, ikitolea mfano utunzaji wa mazingira na uhusiano mzuri uliopo kati ya mgodi huo na jamii inayouzuguka.

“Kwa muda mfupi mmebadilisha mazingira ya mgodi huu. Mnatunza mazingira vizuri, wabunge wamefurahi - na kwa niaba yao ninawapongeza, endeleeni kuwa watunzaji wazuri wa mazingira kwa usalama wa wananchi wetu,” Mwenyekiti wa Kamati hiyo, David Mathayo David alisema wakati wa ziara yao ya kikazi mgodini hapo jana Februari 20, 2024.

Pia waliipongeza Barrick kwa kuendelea kuwa mfano mzuri katika ulipaji wa kodi mbalimbali serikalini, pamoja na kutimiza wajibu wa kutoa mabilioni ya fedha za kugharimia utekelezaji wa miradi ya kijamii kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR).

“Kwenye kampuni kubwa za kiabiasha ninyi [Barrick] mnaongoza kwa kulipa kodi na kutoa gwaio kwa Serikali,” alisema Mathayo.



Kamati hiyo pia ilieleza kuridhishwa na jinsi Kampuni ya Barrick Gold inavyotekeleza Sheria ya ‘Local Content’ na hivyo kuwezesha Watanzania wengi wakiwemo wazawa wanaoishi jirani na migodi yake kunufaika na uwekezaji wake kupitia biashara na ajira, miongoni mwa mambo mengine.

Kwenye ‘Local Content, mmeendelea kufanya vizuri,” alisema Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo ya Bunge imeiagiza Serikali mkoani Mara kuhakikisha tatizo la uvamizi na uporaji wa mawe yenye dhahabu katika Mgodi wa Barrick North Mara linatokomezwa.

“Uwekezaji huu ulindwe, hivi mpaka watu wanabeba mapanga na kuvamia mgodi, vyombo vyetu [vya ulinzi na usalama] vinakuwa wapi, vyombo visaidie kutatua tatizo hili (uvamizi mgodini) kwa sababu tunajirudisha nyuma wenyewe na tunaharibu taswira ya nchi yetu kwa wawekezaji,” Mathayo alionya.



Wakati huo huo, Kamati hiyo imeiagiza Serikali ngazi ya wilaya na mkoa kumaliza pia malamaliko ya wananchi kuhusu mchakoto wa uthaminishaji wa ardhi inayohitajika kwa ajili ya upanuzi wa shughuli za mgodi huo.

Awali, wajumbe wa Kamati hiyo walipata maelezo kuhusu shughuli za uendeshaji wa mgodi huo kabla ya kutembelea sehemu mbalimbali, ikiwemo eneo la majitaka, kinu cha kuchenjua dhahabu na baadhi ya miradi ya kijamii iliyotekelezwa kutokana na fedha za CSR katika vijiji vilivyo jirani na mgodi wa North Mara.

Baadhi ya miradi hiyo ni Shule ya sekondari Matongo, mradi mkubwa wa maji wa Nyangoto na ule wa kilimo biashara unaoendeshwa na vijana katika kijiji cha Matongo.

Meneja wa Barrick nchini Tanzania, Dkt Melkiory Ngido alisema kampuni hiyo kupitia migodi yake ya North Mara na Bulyamhulu imewekeza hapa Tanzania shilingi zaidi ya trilioni sita, na kwamba kati ya kiasi hicho, Serikali imepokea trilioni tatu ambazo zimelipwa kwa mifumo wa kodi na gawio tangu mwaka 2019 ilipokabidhiwa na kuanza kuendesha migodi hiyo kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.



Kuhusu mgodi wa North Mara, Dkt Ngido alisema: “Huu mgodi ulitakiwa kuisha [kufika kikomo] mwaka 2026 lakini kwa juhudi zetu za uwekezaji na za kitaalamu utaenda hadi miaka 15 ijayo - utafika hadi mwaka 2039.”

Kwa mujibu wa Dkt Ngido, Kampuni hiyo pia kupitia mpango wake ujulikanao kama The Barrick-Twiga Future Forward Education Programme imetoa Dola za Kimarekani milioni 30 sawa na shilingi takriban bilioni 70 kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa miundombinu ya shule za sekondari za juu upande wa mabweni na madawati, miongoni mwa mambo mngine katika maeneo mbalimbali nchini.

“Mradi huu upo chini ya TAMISEMI na sisi kama Twiga na Barrick tunafurahi kuunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, ili watoto wote waende A leve (high school),” alisema Dkt Ngido.

Kamati hiyo ya Bunge pia ilielezwa kuwa asilimia 96 ya wafanyakazi takriban 3,000 wa mgodi wa North Mara ni Watanzania, na kwamba juhudi za kuongeza idadi ya wafanyakazi wanawake zinaendelea.

Baadhi ya viongozi waliofuatana na Kamati hiyo katika ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Madini, Dkt Steven Kiruswa, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Kanali Michael Mntenjele, madiwani na wenyeviti wa vijiji kutoka kata tano zenye vijiji 11 vilivyo jirani na mgodi wa Noth Mara.


No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages