
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Kanali Evans Mtambi (katikati), akizungumza katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bunda jana. Wa kwanza kulia ni Mkurugenzi na pili ni Mwenyekiti wa halmashauri hiyo. (Picha na Mara Online News)
Bunda
-------------
Mkuu wa Mkoa (RC) wa Mara, Kanali Evans Mtambi, ameipongeza Halmashauri ya Mji wa Bunda kwa kupata hati safi na kuwataka madiwani kubuni vyanzo vipya vya mapato kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maendeleo.
Kanali Mtambi aliyasema hayo jana mjini Bunda katika mkutano maalum wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Mji wa Bunda ulioketi kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka 2024/2025.
"Mlipata hati safi, hongereni, endeleen kusimamia kazi halmashauri iendelee kupata hati safi. Niendelee kusisitiza kuelekeza mapato ya ndani kukamilisha miradi inayotekelezwa katika bajeti ya 2026/2027,” alisema.
Aliendelea: "Madiwani msimamie ukusanyaji wa mapato ya ndani,,pia kutoa mapendekezo vyanzo vipya vya mapato, ni imani yangu mmejipanga vizuri msipofikia malengo miradi itakuwa ya kusuasua.”
Aidha, Kanali Mtambi aliitaka halmashauri hiyo kuhamasisha na kutoa elimu kwa vijana kujiendeleza kiuchumi kwa kuchukua mikopo ya asilimia kumi, huku akiwataka kuzingatia mfumo wa 4,4,2 kwa kuepuka visingizio visivyo na mashiko.
"Madiwani hamasisheni vijana watumie hii fursa na kuwa wabunifu, fuatilia kama wanakumbana na vizingiti mtoe taarifa tuchukue hatua haraka,” alisema Kanali Mtambi.
Aliitaka halmashauri hiyo kuhakikisha inajibu hoja za CAG na kuziwasilisha serikalini kwa wakati na kuzingatia sheria, kanuni na miongozo kwenye ununuzi wa dawa, vifaa tiba na kufanya utambuzi nyumba ambazo hazina umeme ili wamiliki waweze kulipa kodi ya pango la ardhi.
Pia, kuzingatia nishati safi ya kupikia kwenye taasisi za umma zinazohudumia watu zaidi ya 100 kwa kutumia mapato ya ndani na ruzuku kutoka Serikali Kuu,kutenga na kupeleka fedha za uendeshaji ofisi za mitaa angalau laki mbili kila robo ya mwaka.
Halmashauri hiyo iliahidi kufanyia kazi maagizo yote yalitolewa na Mkuu wa Mkoa kwa ratiba na wakati kwa ajili ya maendeleo na ustawi wa wananchi.
No comments:
Post a Comment