Mfalme Charles III
---------------------------
MFALME Charles III wa Uingereza amegundulika kuugua ugonjwa wa saratani, Buckingham Palace inasema.
Iligunduliwa wakati wa matibabu yake ya hivi karibuni ya tezi dume iliyopanuliwa. Tayari Mfalme huyo ameanza matibabu na ameshauriwa na madaktari wake kuahirisha majukumu ya kiofisi kwa sasa.
Mfalme ana saratani ya aina gani?
Hata hivyo, katika taarifa hiyo iliyotolewa jana Jumatatu, Ikulu haijaweka wazi aina ya saratani inayomsumbua Mfalme Charles III, wala anakopata matibabu.
"Hakuna maelezo zaidi yanayoshirikishwa katika hatua hii, isipokuwa kuthibitisha kwamba Mfalme hana saratani ya kibofu," ilisema taarifa hiyo.
Je, inahusishwa na matibabu yake ya upanuzi wa tezi dume?
Mfalme Charles III mwenye umri wa miaka 75, alitibiwa hivi karibuni kutokana na upanuzi wa tezi dume.
Alikaa siku tatu katika hospitali ya kibinafsi ya Kliniki ya London mwezi uliopita, baada ya kufanyiwa "utaratibu wa matibabu".
Kufuatia hatua hiyo, Ikulu ilisema Mfalme huyo ataahirisha shughuli zake za umma "ili kuruhusu muda wa kupona".
Saratani ni nini?
Saratani hutokea pale seli katika sehemu maalum ya mwili inapogawanyika kwa njia isiyodhibitiwa. Seli hizi zinaweza kuenea kwa tishu zingine za mwili, pamoja na viungo.
Je, unatambuaje saratani?
Kwa kawaida madaktari wataanza kwa kuuliza maswali kuhusu dalili zako. Wanaweza kufanya vipimo. Hiyo inaweza kujumuisha vipimo vya damu na X-ray au vipimo vingine vya picha. Wakati mwingine huchukua sampuli ndogo ya tishu, inayoitwa biopsy, ili kuendesha ukaguzi kwenye maabara.
Mara kwa mara, kama ilivyo kwa Mfalme, saratani hupatikana wakati watu wanaenda kwa uchunguzi wa matibabu kwa mambo mengine.
Uingereza inatoa uchunguzi wa saratani ya matiti, utumbo na shingo ya kizazi. Uchunguzi wa saratani hutafuta dalili za mapema za saratani kwa watu wasio na dalili. Kisha vipimo vingine vinafanywa kuthibitisha utambuzi.
Ni watu wangapi wanapata saratani?
Nchini Uingereza, mtu mmoja kati ya wawili hupata aina fulani ya saratani katika maisha yao.
Kuna zaidi ya aina 200 tofauti za saratani. Zinazojulikana zaidi nchini Uingereza ni matiti, mapafu, kibofu na utumbo, kulingana na tovuti ya NHS UK. Kila saratani hugunduliwa na kutibiwa kwa njia maalum.
Ni matibabu gani maarufu ya saratani?
Kuna njia nyingi tofauti za kutibu au kudhibiti saratani. Inategemea sana aina ya saratani na mahali ilipo.
Baadhi ya saratani zinaweza kuondolewa kwa upasuaji, tiba ya kemikali, yaani chemotherapy ambayo inaweza kutolewa kwa mgonjwa kupitia mshipa, au pia mgonjwa anaweza kumeza tembe za kuua seli za saratani.
Tiba ya mionzi, yaani radiotherapy ni chaguo jingine ambalo wakati mwingine hutolewa. Inatumia miale ya juu ya nishati kushambulia saratani. Hata hivyo, sio matibabu yote yanaweza kuponya.
Je, ni hatua gani tofauti za saratani?
Hatua ni njia ambayo madaktari huelezea ukubwa wa saratani na jinsi imeenea, ambayo inaweza kusaidia katika kuamua matibabu bora zaidi.
Hii inaweza kutumia namba, yaani nambari 11, 2, 3 au 4, ambapo moja inahusu saratani ndogo ambayo haijaenea, ikilinganishwa na nne, ambayo ina maana kwamba ni ya juu na imeenea kote mwilini.
Je, ni watu wangapi wanapona saratani?
Asilimia ya mtu kupona saratani imeongezeka sana katika miaka 50 iliyopita, lakini kiwango cha kuimarika kimepungua katika miaka ya hivi karibuni.
Kulingana na Utafiti wa Saratani UK, nusu ya watu wanaopatikana na saratani huishi na ugonjwa huo kwa miaka 10 au zaidi.
Uwezekano wa kupona saratani kwa kawaida huwa mkubwa kwa watu wanaogunduliwa wakiwa chini ya miaka 40.
Hata hivyo, asilimia ya kupona saratani ya matiti, matumbo na kibofu ni ya juu zaidi katika umri wa kati.
Unapaswa kufanya nini ikiwa unafikiri una saratani?
Inaweza kuwa ya kutisha, lakini unapaswa kuona daktari na kuzungumza juu ya wasiwasi wako.
Dalili unazozipata inaweza isiwe saratani, lakini ni muhimu kufanyiwa uchunguzi. Kugundua saratani mapema kunaweza kurahisisha matibabu. BBC
No comments:
Post a Comment