Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi (katikati) akiwakabidhi makada waliohama upinzani bendera ya chama hicho tawala jana.
---------------------------------------
Mara Online News, Tarime
------------------------------------
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Tarime kimeadhimisha kumbukizi ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa chama hicho tawala, sambamba na kupokea makada waliodai kuhama chama cha upinzani - CHADEMA.
Maadhimisho hayo yalifanyika katika kata Kenyamanyori jana, mgeni rasmi akiwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi.
Chandi alitumia nafasi hiyo pia kuwapokea na kuwakabidhi kadi za CCM wafuasi kadhaa waliohama upinzani, akiwemo kada maarufu Nsenga Werema ambaye ni miongoni mwa waanzilishi wa vyama vya upinzani wilayani Tarime.
Makada waliohama upinzani wakionesha kadi za CCM walizokabidhiwa na Mwenyekiti Chandi.
-----------------------------------------
Walipopewa nafasi ya kuzungumza, wanachama hao wapya wa CCM walisema wameamua kukimbilia chama hicho tawala baada ya kuona upinzani umepoteza dira.
“Nimetazama na kutafakari, ni miaka mingi nimekaa upinzani sioni mwelekeo, nimeamua kurudi nyumbani kaka yangu, Chandi ni ndugu yetu hatuwezi kusimama majukwaa tofauti tukirushiana maneno, sasa tumesimika bendera ya CCM ili kutembea pamoja,” alisema Nsenga.
Aidha, Mwenyekiti Chandi alipokea, kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wananchi wa kata ya Kenyamanyori, zikiwemo za kutorudishwa kwa asilimia 20 za ushuru wa huduma, ubovu wa barabara na migogoro ya ardhi.
Sehemu ya wananchi waliohudhuria maadhimisho hayo
----------------------------------
Kwa upande mwingine, Chandi aliwaomba wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuchagua viongozi wanaotokana na chama tawala - CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika nchini baadaye mwaka huu.
“Mama [akimaanisha Rais Samia Suuhu Hassan] anachapa kazi na zinaonekana, cha kumfurahisha ni viongozi wote watoke CCM katika uchaguzi ujao wa serikali za mitaa. Akina mama jitokezeni kugombea na mmuunge mkono mama mwenzenu [Rais Samia],” alisema Chandi.
Naye Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Tarime, Marwa Daudi Ngicho alisisitiza kuwa CCM ndicho chama pekee chenye majibu ya haja za Watanzania, hivyo wananchi waachane na wapinzani aliowaita “watoa taarifa”.
Mwenyekiti Chandi akikata keki wakati wa sherehe za maadhimisho hayo katani Kenyamanyori jana.
---------------------------------------
No comments:
Post a Comment