Mrajis wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt Benson Ndiege (katikati) akipata maelezo katika banda la mbogamboga na matunda la GHOMACOS katani Natta, wilayani Serengeti jana.
--------------------------------------------
Online News, Serengeti
-------------------------------
MRAJIS wa Vyama vya Ushirika Tanzania, Dkt Benson Ndiege, yuko katika ziara ya kikazi ya kutembelea na kukagua shughuli za vyama hivyo mkoani Mara.
Dkt Ndiege alianza ziara hiyo wilayani Serengeti jana, ambapo alitembelea mnada wa tumbaku, shamba la bustani ya mbogamboga na matunda, soko la bidhaa zinazozalishwa na GHOMACOS na kuzungumza na wakulima.
Katika hotuba yake, alihamasisha wakulima wote kujiunga na vyama vya ushirika ili kupata maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Niwaombe wananchi mjiunge katika ushirika, mtapata pembejeo na masoko, vipato vitaongezeka tofauti na amabvyo utalima mtu mmoja mmoja,” alisema Dkt Ndiege na kuendelea:
“Hakikisheni mnapata elimu, mnasimamia misingi ya chama. Tukijua mipango yenu tutaangalia namna ya kufanya, ninaahidi kushirikiana nanyi.”
Kwa upande mwingine, Mrajis wa Vyama Vya Ushirika, Dkt Ndiege, alitumia nafasi hiyo pia kuwata wakulima wa tumbaku kuacha kutorosha zao hilo la biashara kwenda nchi jirani.
“Acheni kutorosha tumbaku, mtakosesha Serikali mapato, mkiendelea kufanya hivyo pia mtaua ushirika,” alisisitiza Dkt Ndiege.
Awali, alisikiliza kero za wakulima wa tumbaku wa Chama cha Msingi cha Ushirika na Masoko (AMCOS) Ngarawani, zikiwemo za pembejeo kutopatikana kwa wakati, bei ya pembejeo, vifungashio na tumbaku isiyo rafiki kwa mkulima na kutofanyika uchaguzi wa viongozi wa bodi ya chama hicho.
Dkt Ndiege alitoa majibu ya ufumbuzi wa kero za wakulima hao, ikiwa ni pamoja na kumwagiza Mrajis Msaidizi Mkoa wa Mara, Lukas Kiondere kuitisha uchaguzi wa viongozi wa Bodi ya AMCOS ya Ngarawani na kuhakikisha unafanyika kabla ya Aprili mwaka huu.
Mbali na Mrajis Msaidizi huyo, Dkt Ndiege alifuatana na viongozi wengine mbalimbali katika ziara yake hiyo, wakiwemo wa Chama Kikuu cha Ushirika cha Wakulima wa Mara (WAMACU Ltd).
Dkt Ndiege anaendelea na ziara yake leo katika wilaya ya Musoma, ambapo anatembelea mradi wa kukoboa mpunga wa AMCOS ya Inuka na kuzungumza na wanaushirika kabla ya kuelekea wilayani Rorya katika AMCOS ya UWAIRO.
No comments:
Post a Comment