NEWS

Thursday 29 February 2024

Tarime Mji: Waziri Mkuu afurahishwa mradi wa soko la kisasa wenye thamani ya bilioni 9/-Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto) akipewa maelezo ya mradi wa ujenzi wa soko kuu la Tarime Mjini jana Jumatano. Wa tatu kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya Tarime Mji, Gimbana Ntavyo akifuatiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Said Mohamed Mtanda na Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa huo, Patrick Chandi Marwa.
---------------------------------------------

Na Godfrey Marwa, Tarime
------------------------------------


WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la msingi katika mradi wa soko kuu la kisasa linalojengwa katika Halmashauri ya Mji wa Tarime kwa gharama ya shilingi zaidi ya bilioni tisa.

Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali alikagua soko hilo jana Jumatano na kueleza kufurahishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi huo.

“Nimelitembelea soko, nimelioana soko, soko la Tarime ni mwisho. Soko linapamba mji, linafanya Tarime kuwa kivutio,” alisema Majaliwa wakati akihutubia mamia ya wakazi wa mji huo katika uwanja wa Serengeti.

Muonekano wa hatua ya ujenzi iliyofikiwa ya soko hilo - kutoka angani.
------------------------------------
Kwa mujibu wa taarifa iliyosomwa na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Tarime, Gimbana Ntavyo kwa Waziri Mkuu Majaliwa, ujenzi wa soko hilo umefikia asimia 82.

Ntavyo alisema soko hilo likikamilika litakuwa na vibanda vya 325 vya maduka, vizimba 160, bucha tatu, migahawa miwili, benki mbili na ‘Supermarket’ moja.

Aidha, soko hilo litakuwa chanzo kikubwa cha mapato ya ndani ya halmashauri hiyo, ikikadiriwa kuwa litakuwa linaiingizia shilingi milioni 588 kwa mwaka.

Waziri Mkuu anatarajiwa kuhitimisha ziara yake ya siku tano mkoani Mara leo kwa kukagua na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika wilaya ya Musoma.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages