NEWS

Tuesday 13 February 2024

Ziara ya kihistoria: Rais Samia ateta na Papa Francis VaticanRais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Papa Francis jijiji Vatican, Roma.
-----------------------------------------

NA MWANDISHI WETU
------------------------------------


KWA mara ya kwanza, jana Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alikutana na Kiongozi wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis jijini Vatican na kufanya mazungumzo maalumu kwa dakika 25.

Baadaye, Rais Samia alibahatika pia kukutana na kuzungumza na Katibu Mkuu wa Vatican, Kardinali Pietro Parolin aliyekuwa ameambatana na Askofu Mkuu Paul Richard Gallagher ambaye ni Katibu Mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje, Ushirikiano na Mashirika ya Kimataifa.

Taarifa iliyotolewa na Vatican baadaye ilisema viongozi hao walieleza kuridhishwa na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Vatican na Tanzania; mchango na dhamana ya Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Tanzania, hususan katika sekta za elimu, afya na ustawi wa jamii, pamoja na changamoto ambazo Tanzania inapitia kwa sasa.


Rais Samia akipokea zawadi kutoka kwa Papa Francis jijini Vatican.
--------------------------------------
Kisha, walijielekeza zaidi katika masuala ya kijamii nchini Tanzania; masuala ya kikanda na kimataifa na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika kudumisha amani duniani.

Uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Vatican ulianzishwa rasmi Aprili 19, 1968 na Askofu Mkuu Pierluigi Sartorelli ambaye aliteuliwa Balozi wa kwanza wa Vatican nchini Tanzania.

Kwa mujibu wa taarifa ya Vatican, uhusiano huo unajengwa katika misingi ya amani, haki za binadamu, utu, heshima na mshikamano.

Takwimu zilizopo zinaonesha kwamba Kanisa Katoliki nchini Tanzania linamiliki na kuendesha shule za awali 2,490, shule za msingi 147, shule za sekondari 244, vyuo vya ufundi na vyuo vikuu vitano, miongoni mwa taasisi nyingine.

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages