NEWS

Monday 11 March 2024

Hifadhi ya Serengeti yaongoza kwa kutembelewa na wageni wengi TanzaniaSehemu ya watalii katika 
Hifadhi ya Taifa Serengeti
----------------------------------------

NA MWANDISHI WETU, Dodoma
--------------------------------------------


HIFADHI ya Taifa Serengeti inaongoza kwa kuingiza watalii wengi zaidi nchini, amesema Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali, Mobhare Matinyi.

Matinyi aliyasema hayo katika mkutano na waandishi wa Habari jijini Dodoma jana, wakati akitoa taarifa ya maendeleo ya utalii na miundombinu ya hifadhi hiyo baada ya mvua kubwa za el nino.

“Kufuatia mafanikio makubwa ya filamu ya Royal Tour – ambayo Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan alikuwa mshiriki mkuu, idadi ya watalii wanaokuja Serengeti sasa imekwenda juu kupita malengo makubwa yaliyowekwa kwa mwaka huu wa fedha.

“Taarifa ya mafanikio hayo ni kwamba, ingawa makadirio ya idadi ya watalii kwa hifadhi zote za TANAPA kwa mwaka 2023/24 yalikuwa 1,387,987 lakini mpaka kufikia Februari 2024 (miezi nane tu kuanzia Julai 2023), jumla ya watalii 1,451,176 wameshaingia huku Serengeti ikiwa na wengi zaidi,” alisema Matinyi.

Mohbare Matinyi akizungumza
 katika mkutano huo
---------------------------------------
Kuhusu miundombinu ya Barabara, alisema Hifadhi za Taifa 21 zilizo chini ya TANAPA zina barabara zenye urefu wa kilomita 16,470.6, ambapo Serengeti peke yake ina kilomita 3,176 na kwamba kimsingi ndiyo hifadhi yenye mtandao mrefu zaidi wa barabara ambazo ni za udongo ama changarawe.

Barabara hizo zimegawanyika katika barabara kuu zilizo chini ya Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) na kundi la pili la barabara ndogondogo zilizo chini ya TANAPA yenyewe.

Matinyi alifafanua kuwa katika mtandao wa kilomita 3,176 za barabara za Hifadhi ya Taifa Serengeti, kilomita 2,407 ni za udongo na kilomita 769 ni za changarawe, na kwamba kutokana na hoja kadha wa kadha za kiuhifadhi hakuna barabara za lami wala zege.

Aliongeza kuwa Hifadhi ya Serengeti pia ina viwanja vidogo vya ndege (airstrips) vipatavyo saba; ambavyo ni Serengeti, Kogatende, Lobo, Lamai, Grumeti, Kusini na Fort Ikoma.

“Hivyo basi, watalii wanaokuja Serengeti huja ama kwa njia ya barabara au ndege ndogo kutoka maeneo mbalimbali nchini yanayopokea wageni kutoka nje au kutoka kwenye vivutio vingine kama fukwe,” alisema Matinyi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages