NEWS

Tuesday 5 March 2024

Madiwani Halmashauri ya Msalala wazuru mgodi wa Barrick North Mara, waupongeza kwa kujenga uhusiano mzuri na jamii inayouzungukaMadiwani wa Halmashauri ya Msalala wakipata taarifa ya shughuli za Mgodi wa Barrick North Mara baada ya kuwasili mgodini hapo jana.
-----------------------------------------

Na Mwandishi Wetu, Tarime
--------------------------------------


MADIWANI wa Halmashauri ya Msalala iliyopo wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga, wameupongeza Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, kwa kujenga uhusiano mzuri na jamii inayouzunguka.

Pia, wamefurahishwa na ushirikiano uliopo kati ya mgodi huo na viongozi wa kijamii, wakiwemo madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime ulipo mgodi huo unaoendeshwa na Kampuni ya Barrick, kwa ubia na Serikali ya Tanzania kupitia Kampuni ya Twiga Minerals.

Walitoa pongezi hizo jana Machi 5, 2024 walipofanya ziara katika mgodi huo, wakiwa wamefuatana na Mbunge wa Msalala, Iddi Kassim Iddi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Kahama, Thomas Muyonga.


Madiwani wa Halmashauri ya Msalala wakijionea mradi wa majisafi ya bomba uliojengwa kutokana na fedha za CSR Barrick North Mara katika kijiji cha Nyangoto kwa ajili ya matumizi ya wananchi wa vijiji vinne.
----------------------------------------
Katika ziara hiyo, madiwani hao kutoka Halmashauri ya Msalala ulipo mgodi wa Dhahabu wa Bulyanhulu unaoendeshwa pia na Kampuni ya Barrick kwa ubia na Serikali ya Tanzania, walipokewa na uongozi wa Mgodi wa Barrick North Mara, madiwani na wakuu wa idara za Halmashauri ya Wilaya ya Tarime

Pamoja na mambo mengine, walipewa taarifa ya shughuli mbalimbali zinazofanywa na mgodi wa North Mara, kabla ya kupelekwa kujionea miradi ya maendeleo ya kijamii inayotekelezwa na mgodi huo kupitia mpango wake wa Uwajibikaji wa Kampuni kwa Jamii (CSR), kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.

Miradi waliyopelekwa kujionea ni bustani ya kilimo biashara - unaondeshwa na vijana katika kijiji cha Matongo, Shule ya Sekondari Matongo na mradi mkubwa wa majisafi ya bomba uliojengwa kijijini Nyangoto, vilivyopo Nyamongo, kilomita chache kutoka mgodi wa North Mara.

“Tunawapongeza kwa utekelezaji wa miradi hii ya kijamii, viongozi wa mgodi na wananchi endeleeni kushirikiana na kuwa wamoja, na niseme viongozi wa mgodi huu na madiwani mnastahili pongezi kwa kuibadilisha hii wilaya na kupiga hatua kubwa ya maendeleo,” alisema Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Muyonga.


Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Kahama, Thomas Muyonga akizungumza katika kikao cha uongozi wa mgodi wa North Mara na madiwani wa Halmashauri ya Msalala. Aliyekaa mbele ni Makamu Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Flora Sagasaga.
----------------------------------------
Awali, katika hotuba yake ya kuwakaribisha wageni hao kutoka Msalala, Meneja Mkuu (GM) wa Mgodi wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko alisema uhusiano kati ya mgodi huo na jamii inayouzunguka umeendelea kuimarika tangu Kampuni ya Barrick ianze kuuendesha.

“Nina furaha kuona tuna uhusiano mzuri na jamii inayotuzunguka. Zamani hii hali haikuwepo, tangu tuchukue huu mgodi tumekuwa mstari wa mbele kuleta maendeleo kwa jamii, na hii isingewezekana kama tusingekuwa na uhusiano mzuri.

“Nawashukuru viongozi na jamii kwa ushirikiano wanaotupatia na kufanya operations (shughuli) zetu kuwa na tija. Tunaendelea kuboresha uhusiano na kuona jamii inanufaika na mgodi,” alisema GM Lyambiko.


Meneja Mkuu wa Mgodi wa Dhahabu wa Barrick North Mara, Apolinary Lyambiko akizungumza katika kikao na madiwani wa Halmashauri ya Msalala waliozuru mgodini hapo jana.
------------------------------------------
Naye Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi alisema pamoja na juhudi kubwa wanazofanya katika kuboresha huduma za kijamii, bado mgodi huo unakabiliwa na tatizo la kuvamiwa na makundi ya watu kwa ajili ya kupora mawe yenye dhahabu.

Kutokana na hali hiyo, Meneja Uhadi aliendelea kuwaomba viongozi wa Serikali na wa kisiasa wakiwemo madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuusaidia mgodi huo kukomesha tatizo hilo.

Kwa upande wake Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara aliahidi kufanya mkutano na madiwani kwa ajili ya kutafuta namna ya kuwasaidia vijana wanaohusika katika uvamizi huo ili waweze kuachana na vitendo hivyo vya uhalifu.

Hata hivyo Waitara alisema: "Mtu anayekwenda kuvunja fence (uzio) mgodini na kuiba mawe ya dhahabu ni sawa na anayekwenda kuvunja zizi na kuiba ng'ombe, hivyo atashughulikiwa kama mhalifu."


Mbunge wa Tarime Vijijini, Mwita Waitara (mwenye suti) na Meneja Uhusiano wa Mgodi wa Barrick North Mara, Francis Uhadi (wa pili kushoto) wakiongoza ugeni huo kukagua mradi wa Shule ya Sekondari Mantongo jana.
-------------------------------------------

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages