NEWS

Monday 4 March 2024

Chege alivyomwomba Waziri Mkuu miradi ya kijamii na kimkakati Rorya



Waziri Mkuu Kassim Majaliwa (kulia) mbele akifurahia kumsikiliza Mbunge wa Rorya, Jafari Chege wakati kiongozi huyo wa kitaifa alipozuru jimboni humo wiki iliyopita.
----------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
--------------------------------------------


ALIANZA kwa kuishukuru Serikali ya Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, akisema imeiheshimisha wilaya ya Rorya kwa miradi mbalimbali, kisha akawasilisha kwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa maombi ya miradi mingine ya kijamii na kimkakati. Huyu si mwingine bali ni Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Wambura Chege.

Alipopewa nafasi ya kuzungumza mbele ya Waziri Mkuu Majaliwa aliyekuwa katika ziara ya kikazi mkoani Mara wiki iliyopita, Mbunge Chege alisema kwa kipindi cha miaka mitatu ya Rais Samia madarakani, Halmashauri ya Wilaya ya Rorya imeshapokea kutoka Serikali Kuu shilingi zaidi ya bilioni 34 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya afya na elimu pekee.

“Naomba utakaporudi Mheshimiwa Waziri Mkuu utufikishie salamu kwa Rais wetu mpendwa kwa kututengenezea historia ya kutuheshimisha wananchi wa Rorya, mwambie sisi wana-Rorya tunajivunia sana uongozi wake na hatutamwangusha,” Chege alimwambia Waziri Mkuu Majaliwa.

Alisema Serikali pia haijawasahau wananchi wa Rorya katika miradi mingine ya kijamii, ikiwemo miundombinu ya barabara kwani imeshatoa shilingi bilioni 1.4 kwa ajili ya ujenzi wa madaraja ya mto Omaya na mto Mori.

“Mama [akimaanisha Rais Samia] ametuheshimisha pale [kwenye madaraja hayo] na wananchi sasa wanapita kwa kuunganisha tarafa mbili za Suba na Nyancha.

“Lakini pia limejengwa daraja la Kowak, linavusha wananchi, kabla kujengwa wajawazito walikuwa wanapoteza maisha wakati wakijaribu kuvuka kwa mitumbwi. Vile vile Rais ametoa fedha za ujenzi wa daraja la Sakawa, haya yote ni matunda tunayojivunia katika uongozi wake,” alisema Chege.

Alioongeza: “siyo hivyo tu, leo ninavyozungumza tuna shilingi bilioni 134 za mradi mkubwa wa maji ambao unajengwa Rorya katika kata ya Nyamagaro, utakapokamilika tutawagawia na wenzetu wa Tarime. Fedha hizi [bilioni 134] ziliombwa miaka nenda rudi hazikuwahi kuja, lakini kwenye uongozi wa Dkt Samia zimeletwa na sasa zinakwenda kunufaisha wananchi wetu.”

Hata hivyo, Mbunge Chege alitumia nafasi hiyo pia kuiomba Serikali kupitia kwa Waziri Mkuu Majaliwa fedha za kugharimia ukamilishaji wa miundombinu ya Hospitali ya Wilaya ya Rorya na Kituo cha Afya Rabour kwa ajili ya kuhudumia wananchi.

Aidha, Mbunge huyo aliomba suala la wananchi wanaohamishwa kupisha Ranchi ya Utegi limalizwe kwa kuhakikisha wahusika kunapewa stahiki zao ili waweze kuendeleza maisha yao na familia zao.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa wananchi hawa wamekuona hapa wangetamani wajue mstakabali wao uko wapi kwa sababu wameridhia kuondoka katika eneo hilo kwa kutambua kuwa sheria inampa Rais mamlaka ya kutwaa eneo lolote kwa manufaa ya nchi au Taifa,” alisema.

Kwa mujibu wa Chege, kiasi cha shilingi laki moja kwa ekari moja kilichoainishwa kulipwa kwa wananchi hao ni kidogo kwani hakikidhi mahitaji halisi ya kununua na kujenga makazi yao na familia zao katika maeneo mengine.

“Mheshimiwa Waziri Mkuu sisi huku unakuta mtu mmoja ana wake watatu, ana watoto wanne, anafuga mifugo na kulima chakula hapo hapo, hivyo akipewa laki sita ili ahame kutafuta eneo haitoshi kwa thamani ya ardhi ya kwetu huku, laki sita anakwenda kununua eneo la mita za mraba 300 peke yake.

“Hivyo katika hili Mheshimiwa Waziri Mkuu, nikuombe kwa unyenyekevu mkubwa sana tuiongeze hiyo laki sita ili mtu atakapokuwa anahama kutoka eneo hili akienda apate angalau eneo la kumtosheleza na familia yake,” alisema mbunge huyo kutoka chama tawala - CCM.

Pia Mbunge Chege aliomba kujengewa barabara ya lami kuanzia Utegi - Shirati mpaka Kilongwe ambayo alisema imekuwa ikiwekwa kwenye Ilani ya CCM ya Uchaguzi kwa awamu zaidi ya tatu bila mafanikio.

“Ni imani yetu kwamba wakati huu ambao Mama [Rais Samia] anafanya mengi mazuri, barabara hii ya kilomita 56 itajengwa kwa kiwango cha lami ili ikifika 2025 (mwakani) tukiwa tunakinadi chama na Mheshimiwa Rais, angalau barabara hii iwe inapitika vizuri na kunufaisha wananchi,” alisema.

Kwa upande mwingine, Mbunge Chege aliomba kujengewa miradi ya kimkakati kwa ajili ya kuinua mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya na uchumi wa wananchi wake kwa ujumla.

Alitaja miradi ya kimkaka wanayohitaji kujengewa wilayani Rorya kuwa ni soko kubwa la chakula na bidhaa Kilongwe, soko la samaki Shirati, soko la dagaa Utegi, stendi ya kisasa ya magari Ingri Juu na ukamilishaji wa Chuo cha Mafunzo ya Ufundi (VETA) Gabimori kwa ajili ya mafunzo ya uvuvi.

Akijibu maombi hayo ya Chege kwa idhini ya Waziri Mkuu Majaliwa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Deogratius Ndejembi kwanza alimpongeza mbunge huyo kwa jitihada kubwa anazofanya kuwaletea wananchi wa jimbo la Rorya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

“Mheshimiwa Mbunge Chege aliwasilisha hoja binafsi bungeni kuomba Serikali iongeze bajeti ya TARURA, akazungumzia barabara zilizoharibika katika jimbo lake kipindi cha mvua.

“Rais aliposikia kilio kile alielekeza Wizara ya Fedha kutoa fedha za TARURA, na TAMISEMI tulipokea bilioni 30 ya dharura kwa ajili ya kukarabati barabara maeneo mbalimbali nchini. Hapa Rorya kwa jitihada za Mheshimiwa Chege wamepata milioni 250 kwa ajili ya kukarabati barabara zenye changamoto,” alisema Ndejembi.

“Wakati Chege anaingia madarakani kuwa Mbunge wa Jimbo hili la Rorya, bajeti ya TARURA katika wilaya hii kwa mwaka ilikuwa shilingi milioni 778, Dkt Samia alipoingia madarakani sasa Rorya zinakuja takriban shilingi bilioni 3.8 kwa ajili ya ukarabati wa barabara, hii yote ni kazi nzuri anayofanya Mheshimiwa Mbunge Chege.

“Ukiacha barabara, wakati Chege anaingia madarakani kulikuwa na kata ambazo hazikuwa na shule za sekondari, lakini Mheshimiwa Rais alitoa fedha na tayari halmashauri hii [ya Rorya] imepata shule mbili; moja imepata milioni 470 na nyingine milioni 580.

“Pia uwekezaji mkubwa wa bilioni tatu umefanywa na Serikali kwenye ujenzi wa Hospitali ya Wilaya, na katika mwaka wa fedha uliopita zililetwa shilingi milioni 350 kwa ajili ya vifaa tiba.

“Lakini niseme tunayapokea [maombi ya Mbunge Chege ya miradi], lakini ni wajibu wa halmashauri kuandika andiko la kuomba miradi hii na kulifikisha Ofisi ya Rais - TAMISEMI ili uanze mchakato wa kutafuta fedha za kuleta hapa kama miradi ya kimkakati.

“Nimtake Mkurugenzi (Mtendaji) wa Halmashauri aweze kukaa na Afisa Mipango wake na kuona mahitaji yao ya kimkakati na kuleta mara moja maandiko hayo TAMISEMI ili tuweke kwenye mipango ya fedha na kuhakikisha kama alivyoomba hapa Mbunge Chege fedha zinapatikana,” alisema Naibu Waziri Ndejembi.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages