NEWS

Monday 4 March 2024

Mawaziri kurudi tena Nyanungu kusaka suluhisho mgogoro wa bikoni za Hifadhi ya Serengeti na wananchiWaziri Mkuu Kassim Majaliwa akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara katani Nyamwaga, Tarime wiki iliyopita.
------------------------------------------

NA MWANDISHI MAALUMU
-------------------------------------------


MGOGORO wa kugombea mpaka kati ya Hifadhi ya Taifa Serengeti na vijiji vinavyopakana nayo katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime [Vijijini], bado unahitaji mazungumzo zaidi ili kutatuliwa, kwa mujibu wa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Akihutubia wananchi katika mkutano wa hadhara katani Nyamwaga wiki iliyopita, Waziri Mkuu Majaliwa alisema timu ya mawaziri wanane wa kisekta itarudi katika vijiiji hivyo vilivyopo kata za Nyanungu, Gorong’a na Kwihancha, kwa ajili ya majadiliano ya ufumbuzi wa mgogoro huo.

Katika mvutano huo, wananchi wameendelea kulalamika wakipinga uamuzi wa Serikali wa kuweka vigingi vya kutengenisha mpaka wa hifadhi hiyo na kutaka kuwaondoa kwenye amaeneo ambayo wamekuwa wakiishi katika vijiji hivyo vikiwemo Kegonga, Nyandage na Gibaso.

Waziri Mkuu Majaliwa alisema baada ya kupata malalamiko hayo mwaka jana aliwaagiza mawaziri kadhaa wakiwemo wenye dhamana za maliasili, ardhi na TAMISEMI wakaenda kuzungumza na wananchi wa maeneo hayo na watumishi wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).

Hata hivyo, Mtendaji Mkuu huyo wa Serikali alisisitiza kwamba kutokana na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kutaka migogoro ya wananchi na hifadhi itatuliwe nchini kote, mawaziri wanane wa kisekta watarejea katika vijiji hivyo kwa ajili ya tathmini zaidi ili kupata suluhisho la kudumu.

“Mheshimiwa Rais kwenye eneo hili (maeneo yenye migogoro kati ya wananchi nahifadhi) amelifanyia kazi sana kwa kuangalia mgogoro huo una maslahi mapana kwa upande gani - wa wananchi au upande wa hifadhi.

“Kwa hiyo nawasihi wakati timu ya mawaziri inakuja tuendelea kufanya subira waje waangalie, wanakuja mawaziri wote - mazingira, ardhi, maliasili, TAMISEMI wote wanakuja ili waone umuhimu wa uhifadhi wa eneo hilo na mahitaji ya wananchi wetu, halafu tufanye maamuzi… maeneo haya yataangaliwa na mapendekezo yatakayotolewa yatafanyiwa kazi,” alisema Majaliwa.
Chanzo: Gazeti la SAUTI YA MARA
#Ukweli kwa Weledi

No comments:

Post a Comment

Post Top Ad

Your Ad Spot

Pages